Wazayuni wazidi kupapurana, sasa ni zamu ya mkuu wa MOSSAD
Mkuu wa shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni MOSSAD amemshambulia kwa maneno makali waziri mkuu wa utawala huo dhalimu, Benjamin Netanyahu, kwa kukwamisha tena mazungumzo ya kusimamisha vita Ghaza. Kabla ya hapo, mkuu wa majeshi ya Israel naye alikuwa amemshambulia vikali Netanyahu kwa sababu hiyo hiyo.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth, usiku wa kuamkia leo Alkhamisi limemnukuu mkuu wa shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni, David Barnea akisema kuwa, hakufurahishwa na masharti mapya yaliyowekwa na Benjamin Netanyahu katika mazungumzo na makundi ya Palestina.
Ikiwa ni katika kuendeleza njama zake za Kizayuni na kufikiria kwanza nafasi yake ya kisiasa, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu hivi karibuni amekwamisha tena mazungumzo na Wapalestina kwa kuweka masharti mapya ambayo kamwe hayawezi kukubaliwa na wanamapambano wa Palestina. Miongoni mwa masharti hayo mapya ni kutaka vivuko vya Ghaza vya upande wa Misri vidhibitiwe na jeshi la utawala wa Kizayuni, sharti ambalo akili yoyote salama haiwezi kukubaliana nalo.

Mkuu wa Mossad amemlaumu Netanyahu kwa kuweka masharti hayo mapya akisisitiza kuwa, mateka wa utawala wa Kizayuni walioko mikononi mwa wanamapambano wa Palestina hawana muda wa kutosha wa kuvumilia ukwamishaji huo unaofanywa na Netanyahu.
Mkuu huyo wa shirika la kijasusi la Israel ndiye anayeongoza ujumbe wa utawala wa Kizayuni katika mazungumzo ya kusimamisha vita huko Ghaza. Mara nyingi amekuwa akielekea Misri na Qatar kwa ajili ya mazungumzo na makundi ya Palestina na anaamini kuwa ndoto za Netanyahu za kuingamiza HAMAS na kukomboa mateka wa Kizayuni kwa mtutu wa bunduki kamwe haziwezi kuaguka.