HAMAS, Jihadul Islami zaitaka PLO iache kuitambua Israel
Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina za HAMAS na Jihadul Islami zimeitaka Mamlaka ya Ndani ya Palestina ibatilishe uamuzi wake wa kuutambua utawala haramu wa Israel.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa Doha, mji mkuu wa Qatar na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya HAMAS na Katibu Mkuu wa Jihadul Islami, Ziyad al-Nakhalah inasema: Viongozi (wa HAMAS na Jihadul Islami) wanaona kwamba, kwa kuzingatia msimamo wa Knesset uliotangaza kukataa haki ya watu wa Palestina ya kuanzisha taifa lao huru, jumuiya ya kitaifa inatakiwa kuchukua msimamo mmoja kukabiliana na juhudi za kufuta kadhia ya Palestina.
Msimamo huo wa Harakati za Mapambano ya Kiislamu za Palestina za HAMAS na Jihadul Islamu unatolewa baada ya Bunge la Israel (Knesset) siku ya Jumatano kupasisha rasimu ya azimio inayopinga kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina.
Wabunge waliopiga kura ya kupinga kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina ni pamoja na wanaotokea muungano wa vyama vya mrengo wa kulia unaoongozwa na Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu pamoja na chama cha upinzani cha Benny Gantz. Azimio hilo linadai kuwa kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina kunatishia uwepo wa Israel na usalama wa raia wake.
Kadhalika harakati hizo za kupigania ukombozi wa Palestina za HAMAS na Jihadul Islami zimeitaka Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) itangaze kufutwa makubaliano ya nakama ya Oslo, yaliyotiwa saini tarehe 13 Septemba 1993 kati ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na PLO.
HAMAS na Jihadul Islami zimesema, mauaji ya kimbari yanayoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza yanadhihirisha ukweli kwamba, muqawama ndilo chaguo kuu la taifa la Palestina kwa ajili ya kuikomboa ardhi hiyo, kupatikana haki ya kurejea wakimbizi na haki ya Wapalestina kujiamulia mustakabali wao.
Makundi hayo ya muqawama yamesisitiza kuwa, taifa la Palestina linaendelea na mapambano yake halali mkakabala wa vita vilivyoshindwa vya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.