Meshal: Hatutaitambua Israeli, na vitisho havitavunja azma yetu
Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) nje ya Palestina, Khaled Meshaal, amesema kuwa harakati hiyo haitaitambua Israel, na kwamba Hamas haitaathiriwa na vitisho vya aina yoyote.
Meshaal ambaye alikuwa akihutubia katika mji mkuu wa Qatar, Doha, jana Ijumaa, baada ya mazishi ya Ismail Haniyeh na mlinzi wake, alisema: "Hatutalegeza kamba katika misimamo yetu wala hatutaitambua Israeli. Taifa letu litaendelea kulinda umoja wetu wa kitaifa kwa kufuata njia ya Jihadi, mapambano na kurejesha haki zetu.”
Amesema: "Adui zetu (akimaanisha Israeli) hawajifunzi somo. Wameua viongozi wetu tangu miaka 100 iliyopita, lakini nini kimetokea?" Meshal amesema: "Kila kiongozi anapouliwa shahidi, anakuja kiongozi mwingine. Hii inawafanya watu wetu kuwa na nguvu zaidi."
Ameongeza kuwa "maadui hawajui kuwa tunaishi kama mujahidina, na tunakutana na Mola wetu tukiwa mashahidi."
Khaled Meshaal ameongeza kuwa: "Tutaendela kulinda njia yetu. Mashinikizo hayafui dafu kwetu, na vitisho havitavunja irada na azma yetu au kutuondoa katika njia ya malengo yetu hata chembe moja."
Amebainisha kuwa, "Palestina itasalia kuanzia baharini hadi mtoni mwake, na kutoka kaskazini hadi kusini, na Quds (Jerusalem) ni kibla na lengo letu, na hakuna nafasi kwa Wazayuni katika ardhi ya Palestina."