Jeshi la Yemen latungua ndege ya kivita isiyo na rubani ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper
Vikosi vya ulinzi vya anga vya Yemen vimeitungua ndege nyingine ya kivita isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper ya Marekani katika anga ya Yemen.
Msemaji wa Jeshi la Yemen Jenerali Yahya Saree amesema vitengo vya ulinzi wa anga vya nchi hiyo vimefanikiwa kudungua ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani wakati ilipokuwa ikifanya shughuli za uhasama katika anga ya mkoa wa Sa'ada wa Yemen.
Saree amesema katika taarifa ya televisheni siku ya Jumapili kwamba ndege hiyo isiyo na rubani ililengwa kwa kombora la kutoka ardhini kuelekea angani.
Kwa mujibu wa Saree, hiyo ni ndege ya saba ya kivita ya aina hiyo ambayo walinzi wa anga wa Yemen wameiangusha tangu mwezi Oktoba mwaka jana wakati wa kuanza kwa operesheni za kuwaunga mkono wananchi wasio na ulinzi wa Palestina waliozingirwa katika Ukanda wa Gaza.
Msemaji huyo amethibitisha kuwa vikosi vya wanajeshi wa Yemen vitaendelea kuimarisha uwezo wao wa kiulinzi ili kukabiliana na uvamizi wa pamoja wa Marekani na Uingereza dhidi ya nchi yao, na wataendelea na operesheni za kuiunga mkono Palestina hadi vita vya Israel dhidi ya Gaza vitakapokoma na kusitishwa mzingiro dhidi ya Gaza.