Ayatullah Sistani awekwa kwenye orodha ya mauaji ya utawala wa Israel
-
Ayatullah Ali al-Sistani
Idhaa ya 14 ya Israel imechapisha picha ya kiongozi wa juu zaidi ya Kiislamu nchini Iraq, Ayatullah Ali al-Sistani, kama mmoja wa walengwa wa mipango ya mauaji ya kigaidi ya Israel.
Picha ya Ali Sistani ilionekana pamoja na picha za kiongozi wa kundi la Ansarullah, Abdul Malik Al-Houthi, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qassem, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) Yahya Al-Sinwar, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ismail Qaani, na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Ali Khamenei.
Idhaa ya Israel - ambayo iko karibu na Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu - ilichapicha picha hizo jana, Jumanne, zikiambatana na neno "shabaha" kwenye kichwa cha kila mmojawao.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imeripoti kuwa, Israel haijawahi kuzungumza hapo awali kuhusu suala la kumuua kigaidi Ayatullah Sistani, ingawa baadhi ya maafisa wake walitaja majina ya wengine wote ambao picha zao zimeonyeshwa na idhaa hiyo kama "shabaha" kwenye orodha ya mauaji ya Israel.
Ayatullah Ali Sistani - aliyezaliwa mwaka wa 1930 - ni marja' na kiongozi wa ngazi ya juu kabisa wa kidini kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq na maeneo mengine ya dunia na anaishi katika mji mtakatifu wa Najaf katikati mwa Iraq.

Katika majibu yake ya kwanza, Serikali ya Iraq imesema kwamba, inalaani kwa maneno makali hujuma yoyote dhidi ya kiongozi huyo mkuu wa kidini.
Taarifa iliyotolewa leo na serikali ya Iraq, imezitaka taasisi zote za Umoja wa Mataifa na kimataifa kulaani na kukemea jambo lolote linalogusa hisia za Waislamu wote duniani.