Wizara: Israel imeua wanafunzi karibu 12,000 tangu Oktoba 2023
Wizara ya Elimu katika Ukanda wa Gaza imesema utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua wanafunzi zaidi ya 11,852 katika eneo hilo lililozingirwa la Palestina, tangu Oktoba mwaka jana 2023.
Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, wizara hiyo imesema kuwa, wanafunzi wengine 18,959 pia walijeruhiwa tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana.
Kadhalika taarifa hiyo imebainisha kuwa, wanafunzi 114 wameuawa katika eneo la Ukingo wa Magharibi linaokaliwa kwa mabavu, huku 594 wakijeruhiwa katika kipindi hicho.
Aidha takriban walimu na wasimamizi 560 wa shule wameuawa na 3,729 kujeruhiwa huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, mbali na zaidi ya 148 kuzuiliwa katika eneo hilo linalokaliwa kwa mabavu.
Wizara hiyo imesema shule 362 za serikali, vyuo vikuu na majengo yao, na skuli 65 zenya mfungamano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) zimeshambuliwa kwa mabomu na kuharibiwa huko Gaza.
Aidha kwa mujibu wa taarifa hiyo, takriban wanafunzi 718,000 wa Ukanda wa Gaza wamenyimwa fursa ya kwenda shule na vyuo vikuu, huku wanafunzi wengi wakikabiliwa na sonona na kiwewe cha kisaikolojia na matatizo mengine ya kiafya.