Wapalestina 28 wauawa shahidi katika mashambulizi ya Israel Gaza
Makumi ya Wapalestina wameuawa shahidi huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika jinai mpya za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Duru za hospitali zimesema kwa akali Wapalestina 28 waliokimbia makazi yao, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa shahidi katika shambulio la anga la Israel katika eneo la shule katikati mwa Gaza, wakati ambapo utawala wa Kizayuni umeagiza hospitali katika maeneo ya kaskazini zifungwe.
Shambulio hilo la anga jana jioni lililenga shule ya Rafidah huko Deir al-Balah, ambayo ilikuwa na makazi ya watu zaidi ya 1,000 waliokimbia makazi yao kutokana hujuma za kinyama za Wazayuni. Watu zaidi ya 60 pia walijeruhiwa.
Vikosi vya jeshi katili la Israel vimekuwa vikifanya mashambulizi makubwa katika kambi za wakimbizi huko Deir al-Balah, Jabalia, na miji ya karibu ya Beit Hanoun na Beit Lahiya kaskazini mwa Gaza tangu mapema wiki hii.
Kwa mujibu na maafisa wa Wizara ya Afya ya Palestina, watu wasiopungua 130 wameuawa shahidi katika mashambulio hayo ya karibuni, mbali na maelfu ya wengine kujeruhiwa.
Mashambulizi ya umwagaji damu ya utawala huo katili huko Gaza tokeo Oktoba 2023 hadi sasa yameua zaidi ya Wapalestina 42,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine. Maelfu ya Wapalestina pia hawajulikani walipo, na inakisiwa kuwa wamefukiwa chini ya vifusi.