Maji yamfika shingoni Netanyahu; amtimua waziri wa vita, maandamano yashtadi
(last modified Wed, 06 Nov 2024 03:05:52 GMT )
Nov 06, 2024 03:05 UTC
  • Maji yamfika shingoni Netanyahu; amtimua waziri wa vita, maandamano yashtadi

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amemfuta kazi Waziri wa Vita wa utawala huo, Yoav Gallant kutokana na kushindwa kwa utawala huo wa Kizayuni kukabiliana na mrengo wa Muqawama katika Ukanda wa Gaza na Lebanon.

Katika tangazo la kushangaza na kushtukiza Jumanne jioni, ofisi ya waziri mkuu wa Israel imesema kuwa, Netanyahu amemteua waziri wa mambo ya nje wa utawala huo, Israel Katz kuchukua nafasi ya Gallant.

Netanyahu na Gallant wamekuwa wakivutana mara kwa mara kuhusu operesheni ya mauaji ya kimbari ya utawala huo haramu dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

"Kwa bahati mbaya, ingawa katika miezi ya kwanza ya vita kulikuwa na uaminifu na kulikuwa na kazi yenye matunda, katika miezi iliyopita uaminifu huu ulivunjika kati yangu na Waziri wa Vita," amesema Netanyahu.

Maandamano dhidi ya Netanyahu mjini Tel Aviv

Haya yanajiri huku maelfu ya Waisraeli wakifanya maandamano mjini Tel Aviv na miji mingine katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Aidha wapinzani wa Israel wameitisha 'mgomo wa jumla' baada ya Netanyahu kumfukuza kazi Gallant.

Hii ni katika hali ambayo, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Karim Khan ameendelea kuwataka majaji wa mahakama hiyo watoe haraka waranti wa kukamatwa Netanyahu na Gallant.

Tags