Kikao cha "Mahakama ya Gaza" chafanyika London kuwahukumu Wazayuni
Kundi la wanafikra, wanaharakati wa haki za binadamu, maprofesa wa vyuo vikuu na wawakilishi wa vyombo vya habari na mashirika ya kiraia limefanya kikao cha kesi ya mfano mjini London kuuhukumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya watu wa Palestina.
Mahakama hiyo ya kiishara ya London inapangwa kufanya kazi kama mbadala wa mahakama za kimataifa na kuwa jukwaa mwafaka la kuwasilisha malalamiko ya mashirika ya kiraia na kuchunguza uhalifu na unyanyasaji uliofanywa katika vita vya Gaza.
Wanachama wa mahakama hiyo ni pamoja na wanafikra na wanaharakati mashuhuri katika nyanja tofauti kutoka kote duniani.
Hatua ya pili ya kesi hiyo ya kiishara imepangwa kufanyika Mei 2025 huko Sarajevo, mji mkuu wa Bosnia na Herzegovina, ambapo ripoti zilizotayarishwa, taarifa za mashahidi na rasimu za maamuzi vitajadiliwa.
Kuanzishwa kwa mahakama hii kunaonyesha kutoridhishwa watetezi wa Palestina kutokana na uzembe wa mfumo rasmi wa sheria wa kimataifa na mahakama za Umoja wa Mataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai katika kushughulikia jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Wapalestina na vilevile ucheleweshaji, mapungufu na kutokuwepo maendeleo ya taasisi hizo ya kimataifa katika mwelekeo huu.