Jul 25, 2016 04:16 UTC
  • Serikali ya Syria: Tuko tayari kwa ajili ya mazungumzo na wapinzani

Serikali ya Syria imetangaza kuwa, iko tayari kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo na makundi ya wanamgambo kwa shabaha ya kurejesha amani nchini humo na kuhitimisha vita vya miaka 5 katika nchi hiyo.

Afisa mmoja katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Syria ametangaza kuwa, serikali ya Damascus iko tayari kuendeleza mazungumzo ya Wasyria kwa Wasyria bila ya masharti yoyote kwa usimamizi na uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa.

Utayari huo wa serikali ya Syria unatangazwa katika hali ambayo, siku chache zilizopita, Staffan de Mistura, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria alielezea matumaini yake ya kuanza tena mazungumzo ya amani ya nchi hiyo mwezi ujao wa Agosti.

Mazungumzo ya amani ya Syria

Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilifanyika mwanzoni mwa mwaka huu. Hata hivyo mazungumzo hayo yalimalizika pasina ya kufikiwa natija kutokana na kushadidi mapigano na ukiukaji usitishaji vita uliofanywa na makundi yanayoipinga serikali na makundi mengine ya kigaidi. 

Athari ya vita nchini Syria

Syria ilitumbukizwa kwenye mgogoro mkubwa wa ndani mwezi Machi mwaka 2011 kufuatia magaidi wa kigeni kutoka kona mbalimbali za dunia walipomiminwa nchini humo ili kufanya mauaji dhidi ya raia na maafisa wa serikali halali iliyochaguliwa na wananchi ya Rais Bashar al-Assad.

Baadhi ya wakimbizi wa Syria wakipokea misaada

Takwimu rasmi zinaonesha kuwa zaidi ya watu laki nne na elfu sabini wameuawa nchini Syria na nusu ya wakazi milioni 23 wa nchi hiyo wamelazimika kuwa wakimbizi.

Wengi wa wakimbizi hao ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu wamekimbilia katika nchi za jirani na Syria.

Tags