Nov 04, 2023 04:16 UTC
  • Viongozi wa SADC wanakutana Angola leo kujadili amani Congo DR

Viongozi wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanakutana leo jijini Luanda huko Agola, katika mkutano wa dharura unaojadili juhudi za jumuiya hiyo katika kuimarisha amani, ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DEC).

Mkutano huo unafanyika kufuatia mapigano yanayoendelea nchini Congo DR baina ya jeshi la serikali na makundi ya waasi hususan katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.

Mei mwaka huu viongozi wa SADC walikutana mjini Windhoek nchini Namibia na kuridhia nchi wanachama kuiunga mkono serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kushughulikia hali ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo kabla ya uchaguzi mkuu.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali ya Tanzania ilieleza kuwa, ujumbe wa nchi hiyo utaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ataambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba na maafisa waandamizi wa serikali.

Pamoja na mambo mengine, mkutano wa leo wa SADC huko Angola utasisitiza umuhimu wa utashi wa kisiasa kwa nchi wanachama katika kuchangia askari na vifaa vya kijeshi kwa ajili ya Misheni ya Ulinzi wa Amani ya SADC katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (SAMIDRC) kwa kifupi, ambapo hadi sasa nchi tatu pekee ndizo zilizochangia askari na vifaa vya kijeshi katika misheni hiyo.

Mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa SADC umetanguliwa na mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama na kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu na Mawaziri iliyofanyika jana tarehe 3 Novemba.   

Tags