UN: Katika kila nusu saa, mtoto 1 alibakwa mashariki ya DRC
Umoja wa Mataifa umelaani kushtadi kesi za ubakaji na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilizoripotiwa katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka huu; huku makabiliano makali yakiendelea kati ya kundi la waasi la M23 na vikosi vya serikali.
Msemaji wa Shirika la Kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, James Elder, alionya jana Ijumaa kwamba, kiwango cha unyanyasaji wa kingono nchini DRC "hakijawahi kuwa cha juu kama cha sasa".
"Ripoti za awali zinaonyesha kuwa, watoto ni kati ya asilimia 35 hadi 45 ya kesi zipatazo 10,000 za ubakaji na unyanyasaji wa kingono zilizoripotiwa, baina ya Januari na Februari mwaka huu," Elder amewaambia waandishi wa habari huko Geneva, akizungumza kutoka Goma.
"Kwa ufupi, na kwa mujibu wa takwimu za awali, wakati vita vilipopamba moto mwaka huu mashariki mwa DRC, mtoto mmoja alibakwa kila baada ya nusu saa," amesema Elder.
Ameeleza bayana kuwa, kuongezeka kwa unyanyasaji huo dhidi ya watoto katika kipindi cha karibuni mashariki ya DRC si kesi zilizosababishwa tu na mgogoro huo, bali "mgogoro wa kimfumo" uliokita mizizi.
"Ni silaha ya vita na mbinu ya makusudi ya ugaidi. Na inavuruga familia na jamii," ameongeza Elder akisisitiza kwamba, takwimu hizi ni kidokezo tu cha yaliyofichika chini ya wingu la hofu, unyanyapaa, na ukosefu wa usalama.
Afisa huyo mwandamizi wa UNICEF ameongeza kuwa, kesi hizo "zinapaswa kututikisa mioyo. Hakika, zinapaswa kulazimisha kuchukuliwa hatua za haraka na za pamoja."
Tangu Januari mwaka jana, waasi wa M23 wamedhibiti miji ya Goma na Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Maelfu ya watu wameuawa na mamia ya maelfu ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo.