Yemen yasisitiza kukabiliana na hujuma yote ya nchi ajinabi
Muhammad Ali al Houthi mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen ametangaza kuwa nchi hiyo iko tayari kikamilifu kukabiliana na uchokozi wowote dhidi ya Yemen.
Muhammad Ali al Houthi ameeleza kuwa nchi yake iko tayari kwa hujuma yoyote dhidi ya Yemen na imeweka tayari vikosi vyake vyote hasa baada ya vitisho vya hivi karibuni vya utawala wa Kizayuni wa Isarel. Amesema, Yemen itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Al Houthi ameongeza kuwa Marekani, Uingereza na washirika wao katika eneo la Asia Magharibi zinandeleza njama zao dhidi Mhimili wa Muqawama lakini wametambua kuwa hawawezi kutegemea tukio lolote kwa ajili ya kutekeleza malengo yao ya kujitanua nchini Yemen.
Kuhusu sisitizo la Sana'a kwamba iwapo Marekani na waitifaki wake watatekeleza hujuma mpya ndani ya Yemen maslahi yote ya Wamarekani yatashambuliwa, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa Yemen, Abid al-Thawr amesema kuwa: Hatutairuhusu Marekani kuwa yenye taathira zaidi katika matukio ya kikanda na uwezo na nguvu ya kijeshi ya Yemen umefikia kiwango ambayo kinaiwezesha kukabiliana na tukio lolote la kimkakati na kulisambaratisha.
Siku ya Jumatatu iliyopita, jeshi la Yemen lilishambulia maeneo ya kijeshi ya adui Mzayuni katika eneo la "Jaffa", kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa kutumia kombora la balestiki la hypersonic. Jeshi la Yemen lilitekeleza shambulio hilo katika kukabiliana na imashambulizi ya jeshi la Kizayuni dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen.