Mapendekezo matano ya Iran katika mkutano wa D8
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120418-mapendekezo_matano_ya_iran_katika_mkutano_wa_d8
Mapendekezo matano yaliyototolewa na Iran kuhusu nafasi na wajibu wa kundi la "D8" kuhusu Gaza yanaonyesha kuwa, sambamba na matukio ya hivi sasa ya Syria, kuna ulazima wa kuwepo umoja na mshikamano zaidi na zaidi wa nchi za Kiislamu katika kipindi cha sasa, kuliko wakati mwingine wowote, hususan kuhusu masuala ya Palestina.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 21, 2024 09:15 UTC
  • Mkutano wa viongozi wa D8, Cairo
    Mkutano wa viongozi wa D8, Cairo

Mapendekezo matano yaliyototolewa na Iran kuhusu nafasi na wajibu wa kundi la "D8" kuhusu Gaza yanaonyesha kuwa, sambamba na matukio ya hivi sasa ya Syria, kuna ulazima wa kuwepo umoja na mshikamano zaidi na zaidi wa nchi za Kiislamu katika kipindi cha sasa, kuliko wakati mwingine wowote, hususan kuhusu masuala ya Palestina.

Alkhamisi wiki hii, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, aliyekuwa safarini nchini Misri kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa 11 wa wakuu D8, alishiriki pia katika mkutano wa kuchunguza hali ya Gaza na Lebanon, na akaelezea misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu kuhusu matukio ya sasa katika eneo la Asia Magharibi.

Rais Pezeshkian alitoa mapendekezo matano muhimu kuhusu suala la kusitisha vita huko Gaza na kuwasaidia watu wa eneo hilo baada ya vita kumalizika. Mapendekezo haya ni kama ifuatavyo: 1- Kuanzisha mpango wa misaada wa D8 kuhusu Palestina, unaolenga kukidhi mahitaji ya ustawi na ujenzi mpya wa Palestina.

2- Kuunda kundi la mawasiliano la D8 sambamba na kundi la mawasiliano la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa ajili ya kutia nguvu harakati za kimataifa za kusimamisha vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza na kutuma misaada ya kibinadamu ya kimataifa katika eneo hilo.

3- Kuanzisha mfuko wa D8 kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza na Lebanon na kukarabati na kuwawezesha tena wakazi wa maeneo hayo.

4- Uungaji mkono wa wanachama wa jumuiya ya D8 kwa ajili ya kuutambua utawala wa Israel kuwa ni mfumo wa kibaguzi na kufanya juhudi za pamoja za nchi wanachama za kuhuisha azimio nambari 3379 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

5- Kuundwa kamati ya sheria ya pamoja ya wanachama wa jumuiya hiyo kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa Palestina katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), na kuwafungulia mashtaka maafisa wa utawala wa Israel kama wauaji wa zaidi ya watoto elfu 17 wasio na hatia wa Kipalestina.

Pezeshkian akihutubia mkutano wa D8

Mapendekezo hayo matano yametayarishwa kwa njia ambayo inaweza kutumia juhudi na uwezo wa kikanda na kimataifa, huku D8 ikiwa na jukumu la kuratibu na kuunganisha juhudi za pamoja. Kwa msingi huo inaonekana kwamba kuna udharura wa kuundwa sekretarieti ya ufuatiliaji na uratibu wa juhudi za pamoja.

Hapana shaka kwamba, mojawapo ya sababu kuu za kuwasilisha mapendekezo hayo ni nafasi na wajibu wa nchi za Kiislamu kwa ujumla, hasa wanachama wa D8, ambao wanapaswa kuutekeleza kuhusiana na kadhia ya Palestina na mgogoro wa Gaza. Uhalifu wote uliofanyika katika Ukanda wa Gaza umeainishwa kama jinai, ambazo ni pamoja na jinai dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari, na maangamizi ya kizazi, na unaweza kufuatiliwa katika mahakama za kimataifa; lakini licha ya harakati na juhudi zilizofanyika hadi sasa katika uwanja huu bado hakujapatikana matokeo yaliyotarajiwa.

Kuharakisha ujenzi mpya wa Gaza ni haja ya dharura, na kwa kuzingatia ukubwa wa uharibifu uliofanywa na Israel katika eneo hilo, kunahitajika ushirikiano na juhudi za pamoja za nchi mbalimba na si nchi au upande mmoja.

Gaza

Kwa mujibu wa baadhi ya makadirio, ujenzi mpya wa Gaza utagharimu kwa uchache dola bilioni 80 na utachukua miaka kadhaa, na kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, iwapo hali itaendelea kama ilivyo, unaweza kuchukua miongo kadhaa. Kwa sababu hii, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano wa nchi za D8 na kutumia uwezo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC) kwa ajili ya ujenzi mpya wa Gaza.