Sheikh Naim Qassim: Nafasi ya Gaza itasajiliwa katika historia
-
Sheikh Naim Qassim
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amepongeza makubaliano ya kustisha vita katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa nafasi ya Gaza katika kujitolea itasajiliwa katika historia.
Sheikh Naim Qassim amesema: Tunatoa mkono wa pongezi kwa wananchi wa Palestina na Muqawama kwa kufikiwa makubaliano ya kusimamamisha vita ambayo yanadhihirisha kuimarika Muqawama.
Naim Qassim ameongeza kuwa: Mapambano ya ukombozi na watu wa Palestina wamebatilisha mpango mkubwa wa Israel, na Muqawama umepata kile ulichotaka lakini adui ameshindwa kupata alichokusudia na bila shaka historia itasajili nafasi ya Gaza katika kujitolea na kuzima mpango wa adui, Israel.
Katibu Mkuu wa Hizbullah ameendelea kusema: Mapambano ya Hizbullah dhidi ya utawala wa Israel nchini Lebanon yana nafasi katika ushindi wa Gaza na kusisitiza kuwa: Tuliikwamisha Israel kusambaratisha Muqawama nchini Lebanon, na Hiizbullah ya Lebanon itaendelea kusimama kidete dhidi ya mradi wa Marekani na utawala wa Israel.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Naim Qassim ameitaka serikali ya Lebanon kukabiliana barabara na chokochoko za utawala wa Kizayuni wa Israel.