Lebanon yaunda serikali ya kwanza baada ya zaidi ya miaka miwili
(last modified Sun, 09 Feb 2025 07:09:13 GMT )
Feb 09, 2025 07:09 UTC
  • Lebanon yaunda serikali ya kwanza baada ya zaidi ya miaka miwili

Lebanon imeunda serikali yake ya kwanza kamili tangu mwaka 2022, wakati huu ambapo nchi hiyo ya Kiarabu inajitahidi kujenga upya eneo lake la kusini lililoharibiwa na vita; na kuhakikisha usalama unarejea baada ya mapigano kati ya Israel na Harakati ya Muqawama ya Hizbullah.

Rais Joseph Aoun ametangaza leo Jumapili kwamba amekubali rasmi kujiuzulu kwa iliyokuwa serikali ya muda inayoendeshwa na Najib Mikati. Waziri Mkuu mpya wa Lebanon, Nawaf Salam, ameunda serikali hiyo ya kwanza ya nchi hiyo ya Kiarabu baada ya kupita zaidi ya miaka miwili.

Kadhalika ametia saini dikrii pamoja na Waziri Mkuu Nawaf Salam ya kuunda serikali hiyo mpya. Kwa amri hiyo, Baraza la Mawaziri la Salam la watu 24 limechukua rasmi usukani wa serikali.

Katika hotuba yake Jumamosi, Salam aliapa "kurejesha hali ya kuaminiana kati ya raia na serikali, kati ya Lebanon na majirani zake Waarabu, na kati ya Lebanon na jumuiya ya kimataifa."

Aidha ameahidi kutekeleza mageuzi ya kuiondoa Lebanon kutoka katika mzozo wa kiuchumi wa muda mrefu. "Mageuzi ndiyo njia pekee ya wokovu wa kweli," amesisitiza Waziri Mkuu mpya wa Lebanon.

Mnamo Januari 13, Mkuu wa Jeshi, Joseph Aoun aliteuliwa kuwa Rais wa Lebanon, na Salam alipewa jukumu la kuunda serikali mpya. Salam, 71, mwanadiplomasia, jaji, na msomi, amewahi kuwa balozi wa Lebanon katika Umoja wa Mataifa na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).