HAMAS: Wavamizi hawatokuwa salama ndani ya ardhi ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i122836-hamas_wavamizi_hawatokuwa_salama_ndani_ya_ardhi_ya_palestina
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imeuzungumzia mpango wa kutaka kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa Ghaza na kutangaza kuwa wavamizi hawatokuwa salama ndani ya ardhi hiyo ya Palestina.
(last modified 2025-02-17T04:34:01+00:00 )
Feb 17, 2025 04:34 UTC
  • HAMAS: Wavamizi hawatokuwa salama ndani ya ardhi ya Palestina

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imeuzungumzia mpango wa kutaka kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa Ghaza na kutangaza kuwa wavamizi hawatokuwa salama ndani ya ardhi hiyo ya Palestina.

Harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina imeeleza hayo katika taarifa na kusisitiza kuwa Muqawama na msukumo unaopata wa uungaji mkono wa wananchi, wote kwa pamoja wanaelewa vyema hatari ya mipango ya kuhamishwa kwa nguvu, na wanaeleza bayana kwamba, wavamizi hawatokuwa salama ndani ya ardhi ya Palestina.
 
Hamas imeashiria pia hali ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kubainisha kuwa, hivi sasa wavamizi wanatekeleza mpango ulioratibiwa na wa mahesabu maalumu wa kuwahamisha Wapalestina kwa kutumia mbinu ya uchokozi na uvamizi wa kuendelea, kupanua ujenzi wa vitongoji na kutekeleza sheria za kibaguzi.
 
Kwa upande mwingine, harakati hiyo ya Mapambano ya Palestina imetangaza kuwa shambulio la ndege isiyo na rubani lililofanywa jeshi la Kizayuni mashariki mwa mji wa Rafah ni ukiukaji hatari wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Hamas imesema, jinai hiyo inaongezwa kwenye orodha ya ukiukaji wa vipengee vya makubaliano ya usitishaji vita, mfano wa karibuni zaidi ukiwa ni wa kutoruhusu kuingizwa nyumba za dharura na mashine nzito katika Ukanda wa Ghaza.
 
Katika muendelezo wa ukiukaji wa makubaliano hayo ya usitishaji vita huko Ghaza, jeshi la Kizayuni jana liliwaua shahidi kwa kuwapiga risasi maafisa watatu wa polisi waliokuwa wakitoa ulinzi kwa misafara ya ufikishaji misaada ya kibinadamu huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
 
Hamas vilevile imesema, utawala ghasibu wa Kizayuni unachelewesha kuanza kwa awamu ya pili ya mazungumzo, jambo linalothibitisha kuwa hauyapi uzito wala kuyaheshimu makubaliano hayo.../