Watoto wachanga watano wafariki Ghaza kutokana na mgando wa baridi kali
(last modified Tue, 25 Feb 2025 10:59:38 GMT )
Feb 25, 2025 10:59 UTC
  • Watoto wachanga watano wafariki Ghaza kutokana na mgando wa baridi kali

Watoto wachanga watano wamefariki dunia katika Ukanda wa Ghaza kutokana na mgando wa baridi kali katika eneo hilo lililowekewa mzingiro na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuzuiwa kuingizwa misaada ya kibinadamu ikiwemo ya vifaa vya huduma za tiba.

Saeed Salah, Mkurugenzi wa Hospitali ya Patient’s Friends Benevolent Society iliyoko Ghaza, amevieleza vyombo vya habari mapema leo: "watoto tisa walilazwa hospitalini ndani ya muda wa wiki mbili zilizopita kutokana na matatizo ya kiafya yaliyosababishwa na baridi kali, watano kati yao wenye umri kati ya siku moja na wiki mbili wamefariki".
 
Salah amebainisha kuwa mtoto mmoja angali yuko kwenye mashine ya kupumulia kutokana na hali yake mbaya kiafya, huku wengine watatu wakiwa wameruhusiwa kutoka hospitalini.
 
Amesema watoto hao tisa walihamishiwa hospitalini hapo kutoka kaskazini ya Ghaza, ambako watu wengi wamelazimika kuyahama makazi yao na kuishi kwenye mahema kufuatia vita angamizi vya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israeli dhidi ya eneo hilo.
 
Salah ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati ili kuwezesha kuruhusiwa kuingizwa nyumba za dharura zinazohamishika, mahema na mafuta katika Ukanda wa Ghaza kwa ajili ya kuwapatia hifadhi maelfu ya Wapalestina wasio na pa kuishi wakati huu wa msimu wa baridi kali.
 
Kwa mujibu wa ofisi ya vyombo vya habari vya serikali ya Ghaza, karibu Wapalestina milioni 1.5 wamebaki bila makazi baada ya vita vya kinyama vya miezi 15 vilivyoanzishwa na jeshi la Kizayuni dhidi ya eneo hilo tangu Oktoba 7, 2023.../