Utawala wa Kizayuni wafanya njama za kudhibiti misaada inayoingia Ghaza
Maafisa kutoka mashirika matano makubwa ya misaada duniani na Umoja wa Mataifa wameonya leo Alkhamisi asubuhi kuhusu njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kuchukua udhibiti wa moja kwa moja wa misaada ya kibinadamu inayoingia kwenye Ukanda wa Ghaza.
Gazeti la Washington Post limewanukuu maafisa hao wa mashirika matano tofauti ya misaada ya kibinadamu duniani na kuandika: "Israel inafanya njama za kudhibiti moja kwa moja misaada inayoingia huko Ghaza na suala zima la usambazaji wa misaada hiyo."
Ripoti hiyo inasema: "Chini ya mpango wa Israel, ni sehemu moja tu ya kivuko cha Karm Abu Salem, ndiyo itakayoachwa wazi kwa ajili ya kuingia misaada ya kibinadamu huko Ghaza na kwamba mfumo wa kufuatilia misaada hiyo utaanzishwa na viongozi wa Israel kwa ajili ya kudhibiti usambazaji wa misaada ndani ya Ghaza."
Hayo yamekuja huku Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ikisema kwamba imepokea vizuri mpango wa nchi za Kiarabu wa kuikarabati na kuijenga upya Ghaza. Mpango huo ni ule uliopitishwa katika mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu mjini Cairo, Misri. Mpango huo pia unakusudia kuzuia kuondolewa Wapalestina katika eneo hilo lililoko chini ya mzingiro mkali na wa kila upande wa Wazayuni.
Hamas imesema katika taarifa yake kwamba, mkutano wa Cairo umeashiria hatua muhimu kuelekea kupatikana sauti moja ya Waarabu na Waislamu kwa kadhia ya Palestina, hasa wakati huu ambapo Israel inaendelea kushambulia na kuwahamisha watu kwenye makazi yao huko Ghaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na al-Quds.