Hamas yajibu kimantiki bwabwaja mpya za Trump
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123574-hamas_yajibu_kimantiki_bwabwaja_mpya_za_trump
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema upayukaji na vitisho vya Trump vinavuruga makubaliano ya kusitisha mapigano kwani vinauchochea utawala wa Kizayuni wa Israel kutotekeleza wajibu wake.
(last modified 2025-03-06T06:28:36+00:00 )
Mar 06, 2025 06:28 UTC
  • Hamas yajibu kimantiki bwabwaja mpya za Trump

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema upayukaji na vitisho vya Trump vinavuruga makubaliano ya kusitisha mapigano kwani vinauchochea utawala wa Kizayuni wa Israel kutotekeleza wajibu wake.

Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem ameliambia Shirika la Anadolu kwamba makubaliano yalitiwa saini kati ya Palestina na utawala wa Israel, ambayo yalisimamiwa na Washington.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, mateka wote lazima waachiliwe katika hatua tatu na Hamas imetekeleza ahadi zake zote katika hatua ya kwanza, lakini utawala unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina unakwepa kuheshimu ahadi zake katika hatua ya pili.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa makubaliano ya usitishaji vita serikali ya Marekani inabidi iushinikize utawala wa Kizayuni uanze awamu ya pili ya makubaliano hayo.

Msemaji huyo wa Hamas ameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni huenda ukatumia vyema matamshi ya hivi karibuni ya Trump ya kuendeleza mzingiro wa Ghaza na siasa za kuwatesa kwa njaa wakazi wa Ghaza kwa kasi kubwa zaidi.

Ameeleza kuwa, njia bora zaidi ya kuwaachilia huru mateka waliosalia wa Israel ni utawala wa Kizayuni kuingia katika awamu ya pili ya mazungumzo na kuulazimisha utawala huo uheshimu makubaliano yaliyopo.

Leo Alkhamisi asubuhi, rais wa Marekani ametishia kwamba kama Hamas hawatafanya anachosema, hakuna mwanachama yoyote wa Muqawama atabakia salama. Vitisho kama hivyo aliwahi kuvitoa huko nyuma rais huyo mpenda migogoro wa Marekani.