Smotrich: Tunatayarisha mpango wa kuwatimua Wapalestina kutoka Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123720-smotrich_tunatayarisha_mpango_wa_kuwatimua_wapalestina_kutoka_gaza
Waziri wa Fedha wa mrengo wa kulia wa Israel, Bezalel Smotrich, alifichua jana Jumapili kwamba maandalizi yanaendelea ya kuanzisha idara katika Wizara ya Ulinzi ili kuwatimua Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-03-10T03:06:33+00:00 )
Mar 10, 2025 03:06 UTC
  • Smotrich: Tunatayarisha mpango wa kuwatimua Wapalestina kutoka Gaza

Waziri wa Fedha wa mrengo wa kulia wa Israel, Bezalel Smotrich, alifichua jana Jumapili kwamba maandalizi yanaendelea ya kuanzisha idara katika Wizara ya Ulinzi ili kuwatimua Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.

Smotrich, ambaye pia anahudumu kama Waziri wa Nchi katika Wizara ya Ulinzi, amesema katika mkutano wa Knesset kwamba": Tunafanya jitihada za kuanzisha idara ya uhamiaji chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, na Waziri wa Ulinzi, Israel Katz, na bajeti haitakuwa kikwazo."

Kiongozi huyo wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Religious Zionism ameendelea kusema kuwa: "Maafisa wa utawala wa Marekani waliniambia kuwa watu milioni mbili wanaoichukia Israel hawawezi kuruhusiwa kusalia karibu na mipaka yako." 

Bezalel Smotrich

Amesema kuwa Israel inashirikiana na utawala wa Marekani unaoongozwa na Donald Trump kuainisha nchi zitakazopokea watu watakaoondolewa Ukanda wa Gaza.

Itakumbukwa kuwa, mpango wa Marekani na Israel wa kutaka kuwafukuza Wapalestina wa Ukanda wa Gaza katika nchi yao umepingwa vikali na jamii ya kimataifa zikiwemo nchi za Ulaya.  

Vilevile Wataalamu wa sheria za kimataifa wanasema mpango wa Trump wa kutaka kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Ukanda Gaza ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, mpango wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Gaza na kuwapeleka katika nchi jirani ni kuendeleza mauaji ya kimbari kwa kutumia zana za kisiasa.