UN yatoa wito wa kukomeshwa mauaji ya raia nchini Syria
(last modified Mon, 10 Mar 2025 06:59:42 GMT )
Mar 10, 2025 06:59 UTC
  • Volker Turk
    Volker Turk

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk ameonya katika taarifa yake kuhusu ghasia za hivi karibuni magharibi mwa Syria na kutoa wito wa kukomeshwa mauaji ya raia nchini humo.

Katika taarifa hiyo, Volker Turk, amezungumzia kupokea ripoti zinazotia wasiwasi sana za mauaji ya raia, wakiwemo wanawake na watoto nchini Syria na kusema: "Mauaji ya raia katika maeneo ya pwani ya kaskazini magharibi mwa Syria lazima yakome mara moja."

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa: "Tumepokea ripoti za muhtasari wa kunyongwa watu wa makundi ya kidini na kikabila na wahusika wasiojulikana, vikosi vya serikali ya mpito ya Syria, pamoja na watu wanaohusishwa na serikali ya zamani ya nchi hiyo."

Volker Turk ameashiria tamko la maafisa wa serikali ya mpito ya Syria juu ya haja ya kuheshimu sheria na kusema: "Matamshi haya lazima yafuatiwe na hatua za haraka za kivitendo za kuwalinda watu wa Syria, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zinazohitajika kuzuia ukiukwaji wowote na matumizi mabaya ya madaraka na kuwawajibisha wahusika wa jinai hizo."

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba makundi yanayowafanyia ugaidi raia lazima yawajibishwe, na kuongeza kuwa: "Uchunguzi wa haraka, wa uwazi na usiopendelea upande wowote lazima ufanywe kuhusu mauaji na ukiukwaji mwingine wowote wa sheria, na wahusika wa uhalifu huo lazima wawajibishwe kwa matendo yao kwa mujibu wa kanuni na visheria za kimataifa."

Katika siku za hivi karibuni, maeneo ya pwani ya Syria yameshuhudia ongezeko la mivutano na mapigano ya umwagaji damu kati ya vikosi vya usalama vya serikali mpya ya Damascus inayoongozwa na Mohammed al-Julani na wapinzani wa sera zake.