Ndege za Israel zashambulia viunga vya Damascus na kusonga mbele Quneitra
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123894-ndege_za_israel_zashambulia_viunga_vya_damascus_na_kusonga_mbele_quneitra
Israel imefanya shambulizi la anga katika viunga vya Damascus huku vifaru vyake vikiendelea kusonga ndani zaidi ya eneo la kusini-magharibi la Quneitra, ikiwa ni sehemu ya uchokozi wake wa hivi karibuni dhidi ya Syria tangu kuondolewa kwa Rais Bashar al-Assad.
(last modified 2025-03-14T03:22:39+00:00 )
Mar 14, 2025 03:22 UTC
  • Ndege za Israel zashambulia viunga vya Damascus na kusonga mbele Quneitra

Israel imefanya shambulizi la anga katika viunga vya Damascus huku vifaru vyake vikiendelea kusonga ndani zaidi ya eneo la kusini-magharibi la Quneitra, ikiwa ni sehemu ya uchokozi wake wa hivi karibuni dhidi ya Syria tangu kuondolewa kwa Rais Bashar al-Assad.

Taarifa  zinasema ndege za utawala haramu wa Israel zililenga jengo la makazi kaskazini-magharibi mwa Damascus Alhamisi. Video fupi iliyochapishwa na jeshi la Israel ilionyesha mlipuko kando ya jengo hilo ukifuatiwa na moshi mzito. Wataalamu wa afya wa eneo hilo walisema kuwa watu watatu walijeruhiwa katika shambulizi hilo la hivi karibuni.

Mfululizo wa mashambulizi ya anga ya Israel pia ulilenga eneo la Kiswah, kusini mwa Damascus, pamoja na maeneo kadhaa ya jimbo la Dara'a. Wakati huo huo, vikosi vya Israel viliingia zaidi vijijini katika eneo la al-Quneitra kwa kutumia vifaru na magari ya kijeshi na kulipua vituo vya zamani vya kijeshi.

Katika tangazo la dhahiri la malengo ya upanuzi wa utawala wa Kizayuni, mwanachama wa bunge la utawala haramu wa Israel lijulikanalo kama Knesset ya Israel,Boaz Bismuth, ametoa wito wa kuwekwa kwa Syria chini ya udhibiti kamili wa utawala wa Israel. Amesema kuwa Israel haitaruhusu nguvu mpya ya kijeshi kuibuka Syria baada ya kuanguka kwa Assad.

Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesisitiza kuwa vikosi vya Israel vitadumisha uwepo wa kijeshi kwa muda usiojulikana kwenye kilele cha Mlima Hermon na eneo linalouzunguka.

Kikundi cha zamani kinachohusiana na al-Qaeda, Hay’at Tahrir al-Sham (HTS), kilidhibiti Damascus mapema Desemba kupitia mashambulizi makubwa, jambo lililosababisha Israel kutumia fursa ya udhaifu ulioibuka kupeleka vikosi vyake ndani ya eneo la usalama linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa ndani ya Syria.

Hadi sasa, utawala ghasibu wa Israel umekalia kwa mabavu karibu kilomita 600 za ardhi ya Syria tangu kuondolewa kwa Assad.