Israel yaendelea kupata pigo, mashirika makubwa ya ndege yagoma kwenda Tel Aviv
(last modified Fri, 09 May 2025 02:33:22 GMT )
May 09, 2025 02:33 UTC
  • Israel yaendelea kupata pigo, mashirika makubwa ya ndege yagoma kwenda Tel Aviv

Mashambulizi ya Jeshi la Yemen dhidi ya uwanja wa ndege wa Ben Gurion huko Tel Aviv yanaendelea kuutia hasara kubwa utawala wa Kizayuni ikiwa ni pamoja na mashirika mawili maarufu ya British Airways na Air Europa kuendelea kugoma kupeleka ndege zao kwenye uwanja huo wa Israel.

Shirika la Habari la Fars limevinukuu vyombo vya habari vya Israel vikiripoti kuwa Air Europa imerefusha uamuzi wake wa Jumapili wa kusitisha safari zake zote za ndege kutoka Madrid kuelekea Tel Aviv.

Kabla ya hapo shirika la ndege la British Airways nalo lilikuwa limefuta safari zote za ndege kwenda na kutoka Israel.

Shambulio la kombora la siku ya Jumapili lililofanywa na jeshi la Yemen kwenye uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv limesababisha mashirika mengi ya ndege kusitisha safari zao za kuelekea katika maeneo ua Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni na ambayo yamepachikwa jina bandia la Israel.

Siku ya Jumapili usiku, shirika la ndege la Uhispania Air Europa lilifuta safari zake za Jumatatu kutoka Madrid kuelekea Tel Aviv. Baada ya hapo vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa shirika hilo limerefusha uamuzi wake huo. Air Europa ni shirika la ndege la tatu kwa ukubwa nchini Uhispania baada ya yale ya Iberia na Vueling.

Hatua hizo zimechukuliwa kutokana na anga ya Israel kuwa katika hali mbaya kutokana na kuongezeka vitisho vya usalama na mashambulizi kutoka Yemen.

Jumatatu usiku, Kundi la Lufthansa, linalojumuisha ndege za Lufthansa, Swiss Air, Austrian Airlines, Brussels Airlines, na Eurowings, nalo lilitangaza kuwa limeongeza muda wa kusimamisha safari zao za ndege katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni hadi Mei 11.

Shirika la ndege la Ugiriki la Aegean Airlines nalo pia limetangaza kusimamisha safari zake za ndege za kuelekea Tel Aviv. Wizz Air ya Hungary pia ilitangaza kuwa imefuta safari zake za ndege kwenda maeneo ya Palestina hadi Mei 8.

Kwa upande wake Kanali ya 12 ya Televisheni ya Israel imeripoti kuwa idadi ya abiria katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion imepungua kwa kiasi kikubwa kwani mashirika ya ndege ya kigeni yamefuta safari zao.

Kabla ya hapo Televisheni ya Al-Masirah ya Yemen ilinukuu taarifa ya vituo vya udhibiti wa usafiri wa anga vikitangaza kwamba, karibu safari 80 za ndege za kuelekea Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion zilifutwa ndani ya saa 24 baada ya operesheni ya hivi karibuni ya jeshi la Yemen.

Hatua hiyo imefuatia maonyo ya mara kwa mara ya wanajeshi wa Yemen kuhusu kuvipiga viwanja vya ndege vya Israel.