Mufti Mkuu wa Saudia ataka watu wafadhili mauaji Yemen
Mufti Mkuu wa Saudi Arabia amewataka waumini na wafanyabiashara wa Kiislamu nchini humo kutoa mchango wa fedha kwa ajili ya kufadhili mashambulizi ya anga ya utawala wa Riyadh nchini Yemen.
Sheikh Abdul Aziz Al ash-Sheikh, Mufti Mkuu na mwanazuoni mashuhuri wa Saudia ametoa fatwa na kusema kuwa ni 'jukumu takatifu na la kiroho' kwa kila Mwislamu nchini humo kutoa 'sadaka' kwa ajili ya askari wa Aal-Saud wanaofanya mashambulizi nchini Yemen. Amesema askari hao wanahitajia msaada wa kifedha haswa wanaofanya hujuma hizo katika maeneo ya mpakani ya Najran, Asir na Jizan.
Hii si mara ya kwanza kwa Mufti huyo kutoa fatwa zinazokinzana na mafundisho halisi ya Uislamu. Mwezi Juni mwaka huu, Sheikh Abdul Aziz Al ash-Sheikh alitoa fatwa ya kuwapa idhini ya kutotekeleza ibada tukufu ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani wanajeshi wa Saudia wanaoishambulia Yemen
Mashambulizi ya anga ya jeshi la utawala huo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 9,400 hadi sasa nchini Yemen wakiwemo watoto karibu 2,000.
Mashambulizi ya Saudia kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu na kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani na utawala haramu wa Israel, yalianza mwezi Machi mwaka jana kwa lengo la kumrejesha madarakani Abd Rabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyetangaza kujiuzulu na kukimbia nchi.