Aragchi: Haikubaliki kuwa na wasiwasi kuhusu mpango wa nyuklia wa amani wa Iran huku Israel ikiwa na silaha za nyuklia
Iran imekosoa undumakuwili wa jamii ya kimataifa kuhusu silaha za nyuklia, na kusema “haikubaliki” kwa madola ya Magharibi kudai kuwa na wasiwasi kuhusu mpango wa nishati ya nyuklia wa amani wa Iran huku yakifumbia macho silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi ametoa kauli hiyo Jumamosi alipokuwa akihutubia mkutano wa Nne wa Mazungumzo kati ya Iran na Nchi za Kiarabu unaofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu amekumbusha kuwa shughuli za nishati ya nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ni za amani na halali, kinyume kabisa na umiliki wa silaha za nyuklia wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amesisitiza kuwa Iran haitaki kumiliki silaha za nyuklia na kwamba silaha za maangamizi ya umati hazina nafasi katika sera ya usalama ya Tehran.
Waziri huyo wa mambo ya nje ameeleza kuwa Iran ni miongoni mwa waanzilishi wa wazo la ukanda usio na silaha za nyuklia barani Asia, na amezitaka nchi za Magharibi kuacha kutumia undumakuwili katika suala la kuenea kwa silaha za nyuklia.
Ameongeza kuwa, “Iran imejitolea kufungamana na mfumo wa kimataifa wa kutoeneza silaha za nyuklia." Aidha, amekosoa msimamo wa madola ya Magharibi na washirika wao wa kupiga kelele bila msingi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani kwa miongo mingi huku wakipuuza ghala la nyuklia la utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akiashiria tena mpango na silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni na matendo yake ya ukatili na kueneza vita katika eneo la Asia Magharibi, Araghchi amesema, “Uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel unabaki kuwa tishio kubwa zaidi kwa amani katika eneo hili.”
Ameilaumu Marekani kwa kuunga mkono utawala huo bila kikomo na kwa nguvu, akiitaja Washington kuwa mshirika katika uhalifu wa utawala huo, hasa jinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina.
Waziri huyo amesema hatua za sasa za kikatili na za mauaji ya kimbari zinazotekelezwa na utawala huo kuwa ni jaribio la moja kwa moja kufuta kabisa uwepo wa taifa la Palestina.
Aragchi amekosoa kile kinachoitwa “suluhisho la mataifa mawili” kuwa ni njama inayotumika kuchelewesha haki za Wapalestina kwa miongo mingi. Amekumbusha kuwa utawala huo wenyewe umeshakataa hata uwezekano huo suluhisho hilo.