Jenerali wa zamani aonya: Israel imegeuka kutoka kuwa mali na kuwa mzigo kwa Marekani
Kamanda wa zamani wa jeshi la Israel huko Gaza amesema Israel sasa imegeuza kutoka kuwa mali na kuwa mzigo mzito kwa Marekani.
Yisrael Ziv, kamanda wa zamani wa kitengo cha jeshi la Israel huko Gaza, alitangaza jana Jumatatu kwamba: "Benjamin Netanyahu ametuingiza kwenye vita visivyoisha kutokana na migogoro ya kisiasa inayomuandama, na sasa Donald Trump anataka kuiweka kando Israel kwa njia yake."
Awali Televisheni ya Israel ilikuwa imeripoti makubaliano kati ya Hamas na serikali ya Marekani bila kushirikisha au kushauriana na Tel Aviv, na kusisitiza kuwa kwa makubaliano hayo, Rais wa Marekani Donald Trump amemzaba kofi Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Chombo hicho cha habari cha Israel kimeongeza kusema katika ripoti hiyo kwamba: "Kwa makubaliano haya ya moja kwa moja na yasiyo na kifani kati ya Hamas na serikali ya Marekani ya kuachiliwa huru Edan Alexander, Mmarekani-Muisraeli, Trump sio tu amempiga makofi Netanyahu bali pia ameihalalisha Hamas na kuipa ushindi ambao hauna kifani tangu mwanzo wa vita."