Rais Trump wa Marekani awasili Saudia, alenga kutoka na kitita cha dola trilioni 1
Rais wa Marekani, Donald Trump, amewasili mjini Riyadh katika awamu ya kwanza ya ziara yake ya siku nne katika eneo la Asia Magharibi, ambapo analenga kupata hadi dola trilioni moja za uwekezaji kutoka Saudi Arabia.
Trump alipokelewa na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid, jijini Riyadh, asubuhi ya Jumanne.
Saudi Arabia ni kituo cha kwanza cha ziara yake ya kimataifa tangu aanze muhula wake wa pili kama rais wa Marekani.
Ripoti zinaeleza kuwa Trump anatarajiwa kusaini mikataba ya thamani ya zaidi ya dola trilioni moja wakati wa ziara yake katika taifa hilo la Ghuba ya Uajemi ambalo ni tajiri kwa mafuta.
Duru zinadokeza kuwa makubaliano hayo yanajumuisha uwekezaji katika makampuni ya teknolojia ya akili mnemba, uzalishaji wa nishati, pamoja na ununuzi wa silaha kutoka kwa watengenezaji wa zana za kijeshi wa Marekani.
Ripoti za awali zimedokeza kuwa Marekani haishinikizi tena Saudi Arabia kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel kama sharti la kuendeleza mazungumzo ya ushirikiano wa nyuklia na ufalme huo.
Mnamo mwaka 2017, Trump alichagua Saudi Arabia kama nchi yake ya kwanza kuitembelea akiwa rais, ambapo alipata ahadi ya uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 450 kwa ajili ya uchumi wa Marekani.
Ziara hiyo pia itamfikisha Trump nchini Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Akiwa Qatar, Trump anatarajiwa kupokea zawadi ya ndege ya kifahari aina ya Boeing 747 ya thamani ya dola milioni 400, itakayotumika kama ndege rasmi ya rais wa Marekani – Air Force One.
Alipoulizwa iwapo atapokea zawadi hiyo kutoka Qatar, Trume amesema: “Wanatupatia zawadi,” na nitakuwa mpumbavu kama sitaikubali."
Mbunge wa Marekani, Ritchie Torres, ameitaka Ofisi ya Uwajibikaji wa Serikali (GAO) kufanya uchunguzi, akisema ndege hiyo inaweza kuwa “zawadi ya thamani kubwa zaidi kuwahi kutolewa kwa rais na serikali ya kigeni.”