Wapalestina 26 wamekufa kwa njaa Ghaza katika muda wa saa 24 zilizopita
(last modified Wed, 21 May 2025 10:11:04 GMT )
May 21, 2025 10:11 UTC
  • Wapalestina 26 wamekufa kwa njaa Ghaza katika muda wa saa 24 zilizopita

Shirika moja la kimataifa la kutetea haki za binadamu limesema kuwa, takriban Wapalestina 26, wakiwemo watoto wadogo 9, wamekufa kutokana na njaa na ukosefu wa msaada wa matibabu katika Ukanda wa Ghaza unaozingirwa kila upande, kwenye kipindi cha saa 24 zilizopita.

Shirika la Kufuatilia Haki za Kibinadamu la Euro-Med limesema kuwa, ongezeko kubwa la vifo miongoni mwa wazee, wagonjwa na watoto linachangiwa na hali mbaya ya maisha iliyosababishwa kwa makusudi na utawala wa Kizayuni kwa lengo la kudhoofisha na kuwadhuru watu.

Shirika hilo lenye makao yake mjini Geneva Uswisi limesema, masharti magumu yaliyowekwa na Israel ni pamoja na kuwaadhibu kwa njaa ya makusudi, kuwapa mateso makali na kuwanyima huduma za matibabu wananchi wa Ghaza.

Euro-Med imeonya kuwa kukosekana mfumo thabiti wa ufuatiliaji ndani ya Wizara ya Afya ya Ghaza kutokana na vikwazo vikali, kumesababisha vifo vingi kwa watu wasio na hatia na raia wa kawaida kutoripotiwa ipasavyo.

Euro-Med pia imetahadharisha kwamba kulazimishwa watu wa Ghaza kuhama maeneo yao kutokana na mashambulizi makali ya mabomu kunazidisha mgogoro wa njaa na kusababisha wakazi wa ukanda huo kupoteza akiba yao ndogo ya chakula cha makopo waliyo nayo.

Shirika hilo la kimataifa la haki za binadamu limeyahimiza mataifa yote kutimiza wajibu wao wa kisheria na kuchukua hatua za haraka za kukomesha mauaji ya umati yanayoendelea kufanywa na Israel katika Ukanda wa Ghaza.

Jeshi katili la Israel lilianzisha tena mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu wa Ghaza tarehe 18 Machi mwaka huu na kuua maelfu ya Wapalestina na kujeruhi wengine wengi.