Ireland yasisitiza Israel inatekeleza mauaji ya kimbari Gaza
Katika mjadala mkali uliotikisa bunge la Ireland, naibu waziri mkuu Simon Harris, ametetea msimamo wa serikali kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la kitaifa la Ireland , RTE, akijibu hoja ya mbunge wa kujitegemea, Catherine Connolly, Harris alisema wazi bungeni kuwa: “Sisi ndio serikali ya kwanza katika Umoja wa Ulaya kusema wazi kuwa kile ambacho Israel inafanya Gaza ni mauaji ya kimbari. Ni mauaji ya kimbari.”
Connolly alikosoa vikali serikali kwa kile alichokiita kutofanya juhudi za kutosha kuiwajibisha Israel, katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza kwa miezi 19 sasa , ambavyo kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, tayari vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 54,000, zaidi ya nusu yao wakiwa watoto.
Harris alisema kwa uchungu:
“Ninasikitishwa na kuchukizwa – kuchukizwa kabisa – kuona watoto wakifa kwenye runinga zetu kila siku. Na ninapokuja kazini kila siku, nafanya kazi kwa ushirikiano na wenzangu hapa kuonyesha uongozi katika kipindi hiki cha vita vya maangamizi.”
Mwaka mmoja uliopita, Ireland ilitambua rasmi taifa la Palestina, na mnamo Januari mwaka huu, iliungana na Afrika Kusini katika kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague.
Kwa mujibu wa gazeti la Irish Times, Harris alieleza kuwa mswada wa kuzuia biashara ya bidhaa kutoka katika makazi ya walowezi Waisraeli , ambayo kisheria ni haramu kimataifa , utawasilishwa kwa Kamati ya Mambo ya Nje mwezi ujao.
Aidha, serikali ya Ireland iko chini ya mashinikizo kutoka kwa makundi ya kiraia na wabunge kufuta ushiriki wa Benki Kuu ya Taifa katika kuruhusu uuzaji wa "Dhamana za Kifedha za Israel" ndani ya Umoja wa Ulaya,, na pia kupiga marufuku ndege zinazobeba silaha kuelekea Israel kuruka katika anga ya Ireland.
Harris ameliambia bunge la Ireland kuwa: “Najivunia wananchi wa taifa hili. Najivunia kuwa tulipoingia kwenye uchaguzi haikujalisha ulikuwa chama gani , wote tulisimama na kusema: ‘Tutasimama na watu wa Palestina.’”
Msimamo wake huo umeungwa mkono mapema wiki hii na Waziri Mkuu, Micheál Martin, ambaye pia alisisitiza msimamo wa serikali kuhusu Palestina alipohutubia bunge la Ireland ambalo linajulikana kama Dáil Éireann.
Martin alisema: “Tumekuwa thabiti tangu mwanzo katika kuunga mkono watu wa Palestina na haki yao ya kujiamulia mambo yao wenyewe, pamoja na kulaani uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari yanayoendelea hivi sasa.”