Aug 06, 2016 06:59 UTC
  • Rais Putin: Hakuna makundi mazuri ya kigaidi

Rais Vladimir Putin wa Russia ameonya dhidi ya kuyatumia baadhi ya magenge ya kigaidi kwa maslahi ya kisiasa na kuyaorodhesha kama makundi mazuri ya kigaidi.

Rais wa Russia ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Azertac la Azerbaijan na kuongeza kuwa, ni jambo lisilokubalika na la hatari mno ni kuyagawa makundi ya kigaidi katika sehemu mbili; magaidi wazuri na magaidi wabaya. Amesema kama tunavyomnukuu: "Ni undumakuwili kuyatumia baadhi ya makundi ya kigaidi kusukuma maslahi ya kisiasa na kijiografia, hauwezi kudai kuwa kuna makundi mazuri ya kigaidi na makundi mabaya ya kigaidi."

Rais Putin wa Russia anasisitiza kuwa hakuna magaidi wazuri

Rais Vladimir Putin amesisitiza kuwa, kwa miaka kadhaa iliyopita ulimwengu umeshuhudia njama za kutaka kudhoofisha serikali katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati, kuzidisha matatizo ya kiuchumi na kijamii sambamba na kupanua zaidi makundi yenye mitazamo mikali.

Matamshi ya Rais wa Russia yanaonekana kuwa radiamali kwa tabia ya Marekani ya kuyagawa makundi ya kigaidi nchini Syria katika makundi mawili, magenge ya magaidi wazuri na wabaya.

Ugaidi wa Marekani nchini Syria

Kwa mara nyingine tena amekariri kuwa, wananchi wa Syria tu ndio wanaoweza kujichukulia maamuzi kuhusiana na mustakbali wa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali na wananchi wa Syria wakiwa na azma na irada thabiti wamesimama kidete katika njia ya kupambana na uwepo wa magaidi wanaotenda jinai katika nchi yao.

Tags