UNRWA: Israel inawatesa raia kwa njaa Ghaza, wakiwemo watoto milioni moja
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128550-unrwa_israel_inawatesa_raia_kwa_njaa_ghaza_wakiwemo_watoto_milioni_moja
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kwa mara nyingine tena limeushutumu utawala wa kizayuni wa Israel kwa kutumia njaa kama silaha ya vita dhidi ya raia Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2025-07-20T11:07:51+00:00 )
Jul 20, 2025 09:45 UTC
  • UNRWA: Israel inawatesa raia kwa njaa Ghaza, wakiwemo watoto milioni moja

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kwa mara nyingine tena limeushutumu utawala wa kizayuni wa Israel kwa kutumia njaa kama silaha ya vita dhidi ya raia Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Katika taarifa iliyoweka kwenye mtandao wa X, UNRWA imesema: "Mamlaka za Israel zinawatesa kwa njaa raia huko Ghaza. Miongoni mwao ni watoto milioni 1."

Shirika hilo la UN limerudia tena kutoa wito wake wa dharura wa kuondolewa mzingiro unaoendelea kuuweka utawala wa kizayuni dhidi ya Ghaza likisema: "Ondoeni mzingiro: iruhusuni UNRWA ilete chakula na dawa."

Licha ya wajibu ilionao wa kisheria wa kimataifa wa kulinda raia na kuruhusu ufikishwaji misaada, tangu Machi Pili, Israel imekuwa ikiendeleza mzingiro na vizuizi dhidi wakazi wa Ghaza, sambamba na kuripua kwa mabomu misafara ya magari ya misaada, kufunga vivuko vya mpakani, na kulenga vituo vya ugawaji misaada; vitendo ambavyo vimelaaniwa vikali, vikielezewa kuwa ni utoaji adhabu kwa Wapalestina wote na uhalifu wa kivita.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Ghaza, makumi ya watoto tayari wameshafariki dunia kutokana na njaa na upungufu wa maji mwilini, wakati mamia ya maelfu zaidi wako hatarini kutokana na kushtadi uhaba wa chakula na kusambaratika kwa mfumo wa utoaji huduma za afya.

Duru za Palestina zimeripoti kuwa, siku ya Jumamosi pekee, mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa kizayuni yaliua Wapalestina wasiopungua 136, wakiwemo watu 38 waliokuwa wakisubiri msaada pamoja na watoto watatu waliofariki kutokana na utapiamlo mkali.

Hadi sasa utawala ghasibu wa Israel umewaua shahidi karibu Wapalestina 59,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, huko Ghaza tangu ulipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo mnamo Oktoba 2023…/