Zaidi ya makundi 100 ya misaada yatahadharisha njaa kali Gaza
Zaidi ya mashirika 100 ya misaada ya kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yametahadharisha kuhusu njaa kali katika Ukanda wa Gaza na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo.
Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), Save the Children na Oxfam ni miongoni mwa asasi zilizotia saini taarifa ya pamoja inayosema wenzao na watu wanaowahudumia "wanadhoofika".
Mashirika hayo yametoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja, kufunguliwa kwa vivuko vyote vya mpaka, na kuruhusu uingiaji huru wa misaada unaoongozwa na Umoja wa Mataifa. Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, theluthi moja ya wakazi wa Ukanda wa Gaza hawajala kwa siku kadhaa kutokana na mzingiro unaoendelea kuwekwa na utawala wa kizayuni wa Israel kwenye eneo hilo la Palestina.
Wakati walimwengu wote wanapaza sauti kuelezea hali mbaya ya njaa inayowakabili wakazi wa Gaza na hata video na picha zinazoenea mitandaoni zinathibitisha hilo, utawala ghasibu wa Israel unakanusha kuhusika na uhaba mkubwa wa chakula. Ripoti zinasema kuwa, Wapalestina wa Ukanda wa Gaza ambao wamenusurika na mashambulizi ya mabomu na risasi za wanajeshi wa Israel sasa wanataabika kwa baa la njaa.
Tangu Machi Pili, utawala ghasibu waIsrael umefunga vivuko vyote vya kuingilia Ghaza, na kusitisha uingizaji wa chakula, dawa, na misaada ya kibinadam katika eneo hilo la Palestina linalokabiliwa na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyoanzishwa na utawala huo wa kizayuni tangu Oktoba, 2023.