Singapore iko tayari kulitambua taifa la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128952-singapore_iko_tayari_kulitambua_taifa_la_palestina
Wakati mpango wa "mataifa mawili" ukisonga mbele katika Umoja wa Mataifa, unaotaka kuanzisha taifa huru la Palestina, serikali ya Singapore imetangaza kuwa iko tayari kutambua taifa la Palestina.
(last modified 2025-07-31T00:44:06+00:00 )
Jul 31, 2025 00:44 UTC
  • Singapore iko tayari kulitambua taifa la Palestina

Wakati mpango wa "mataifa mawili" ukisonga mbele katika Umoja wa Mataifa, unaotaka kuanzisha taifa huru la Palestina, serikali ya Singapore imetangaza kuwa iko tayari kutambua taifa la Palestina.

Mwakilishi wa Singapore katika mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, Kevin Cheuk, amesema nchi yake iko tayari kulitambua taifa la Palestina, na jambo la msingi ni kwamba hatua hiyo inapaswa kuchangia maendeleo kuelekea amani na suluhisho la mataifa mawili.

 Taarifa iliyowasilishwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa mjini New York, ilisema Singapore pia inafikiria kutuma timu ya madaktari katika Ukanda wa Gaza kusaidia kutibu wagonjwa wa ukanda huo. Kevin Cheuk aliongeza kuwa katika muda mrefu, Singapore iko tayari kuchangia ujenzi wa Gaza mara tu makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano yatakapofikiwa.

"Singapore imekuwa ikiunga mkono mara kwa mara haki ya Wapalestina ya kuwa na ardhi ya asili kwa msingi wa suluhisho la mataifa mawili, kwa mujibu wa maazimio husika ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Tunaamini kwa dhati kwamba hii ndiyo njia pekee mwafaka ya kufikia suluhu la kina, la haki na la kudumu kwa mzozo huu wa muda mrefu," alisema.

Mpaka sasa, zaidi ya mataifa 140 wanachama wa Umoja wa Mataifa tayari yametambua taifa la Palestina, huku Hispania, Ireland, na Norway zikijiunga na orodha hiyo mwaka jana. Wakati huo huo, mkutano wa kuhusu suala la Palestina na suluhu la nchi mbili umemalizika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York baada ya siku mbili za majadiliano. Ukiongozwa na Ufaransa na Saudi Arabia, mkutao huo ulilenga kufufua suluhisho la serikali mbili, chaguo la kidiplomasia ambalo linaonekana kuwa mbali zaidi kuliko hapo awali.