Wanajeshi 16 wa Israel wamejiua mwaka huu
Wanajeshi wasiopungua 16 wa utawala wa kizayuni wa Israel wanaripotiwa kujiua tangu kuanza mwaka huu (2025).
Vyanzo vya habari, vikitoa mfano wa ongezeko la matatizo ya afya ya akili miongoni mwa wanajeshi wa Israel, vimeripoti kuwa wanajeshi 16 wa Israel wamejiua tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Mtandao wa Kizayuni wa Kan umetangaza katika ripoti yake kwamba, tangu mwanzoni mwa mwaka huu, askari 16 wa Kizayuni wamejiua, 8 kati yao walikuwa kazini, 7 walikuwa askari wa akiba na 1 ni askari wa kudumu.
Kulingana na takwimu, wanajeshi 21 walijiua mnamo 2024, wakati mnamo 2023 idadi hii ilikuwa 17. Jeshi la utawala wa Kizayuni hadi sasa limekataa kutoa takwimu za idadi rasmi ya askari wake waliojiua, licha ya kuahidi mara kadhaa kuwa litafanya hivyo.
Ripoti ya Yedioth Ahronoth imeeleza kuwa, maelfu ya askari wanatafuta msaada katika kliniki za tiba ya matatizo ya akili, huku karibu theluthi moja ya walioathirika wakionyesha dalili za ugonjwa wa mfadhaiko wa baada ya kupatwa na kiwewe.
Tangu Oktoba 7, 2023 jeshi la utawala wa Kizayuni limeanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza, kwa malengo yanayodaiwa kuwa ni kuiangamiza Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na kuwakomboa mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na Muqawama wa Palestina huko Ghaza. Licha ya kila aina ya vitendo vya kishenzi na kinyama ulivyofanya katika eneo hilo tangu wakati huo hadi sasa, yakiwemo mauaji ya kimbari Wapalestina wapatao 60,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, utawala ghasibu wa Israel mpaka sasa hivi haujaweza kufikia hata moja kati ya malengo hayo.