Sheikh Qassem: Hizbullah kamwe haitasalimu amri au kukabidhi silaha zake
-
Sheikh Naim Qassem
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qassem amesema harakati hiyo ya muqawama kamwe haitakubali kukabidhi silaha zake kwa Israel.
Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kuwa, silaha hizo ni muhimu kwa ajili ya kulindai mamlaka ya kitaifa ya Lebanon mbele ya uvamizi wa utawala wa Tel Aviv.
Sheikh Naim Qassem aliyasema hayo katika hotuba yake iliyotangazwa na televisheni kutoka mji mkuu wa Lebanon, Beirut, Jumatano.
Alisema wale wanaotaka kunyang'anywa silaha za Hizbullah wanatumikia maslahi ya Israel, na wanajifungamanisha na adui Mzayuni.
Amelaani juhudi zinazofanyika ili kupokonya silaha za Hizbullah akizitaja kuwa ni kujisalimisha kwa Israel, na kusisitiza haja ya umoja wa kitaifa, ulinzi na ujenzi mpya.
"Wito wowote wa kutupokonya silaha una maana ya kudhoofisha nguvu ya Lebanon. Kuipokonya silaha Hizbullah kutaiwezesha Israel kupanua uvamizi wake na kudhibiti ardhi ya Lebanon," amesema Sheikh Qassem.

Ameonya kwamba Lebanon inakabiliwa na tishio - sio tu kutoka kwa Israel, bali pia kutoka kwa Marekani na kundi la kigaidi la Daesh, chini ya kivuli cha "Mashariki ya Kati Mpya."
Sheikh Naim Qassem amesisitiza kwamba adui Israel hataishia katika kukalia kwa mabavu maeneo matano muhimu kusini mwa Lebanon, na anasubiri kupokonywa silaha na Hizbullah ili kupanua shughuli zake za ujenzi wa vitongoji haramu.