Hamas yamjibu Netanyahu: Gaza itasalia kuwa mwiba kwa utawala vamizi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129288-hamas_yamjibu_netanyahu_gaza_itasalia_kuwa_mwiba_kwa_utawala_vamizi
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kuwa matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusu kukaliwa kwa mabavu Ukanda wa Gaza ni kubatilisha waziwazi mwenendo wa mazungumzo, na yanafichua nia ya kweli ya kujiondoa kwake katika duru ya mwisho ya mazungumzo, licha ya kukaribia makubaliano ya mwisho.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 08, 2025 04:19 UTC
  • Wapiganaji wa Hamas
    Wapiganaji wa Hamas

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kuwa matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusu kukaliwa kwa mabavu Ukanda wa Gaza ni kubatilisha waziwazi mwenendo wa mazungumzo, na yanafichua nia ya kweli ya kujiondoa kwake katika duru ya mwisho ya mazungumzo, licha ya kukaribia makubaliano ya mwisho.

Harakati hiyo imefafanua katika taarifa iliyotolewa Alhamisi jioni kwamba "kile mhalifu wa kivita, Netanyahu, anachopanga ni kuendeleza mbinu yake ya mauaji ya kimbari na kuwafukuza Wapalestina katika nchi yao kwa kufanya uhalifu zaidi katika Ukanda wa Gaza."

Hamas, ambayo wapiganaji wake na wa makundi mengine ya ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza wamelisababishia hasara kubwa jeshi la Israel, imesisitiza kwamba "Gaza itasalia kuwa mwiba kwa utawala vamizi na majaribio ya kuliweka eneo hilo chini ya usimazi wa kigeni."

Taarifa ya Hamas imesisitiza kwamba "kupanua uchokozi dhidi ya watu wetu wa Palestina haitakuwa safari ya kwenda matembezi katika bustani, na gharama yake itakuwa nzito na kubwa kwa utawala vamizi na jeshi lake la Kinazi."

Hamas imeeleza kuwa mpango wa Netanyahu wa kuikalia kwa mabavu Gaza "unathibitisha pasipo shaka yoyote kwamba anataka kuwatoa kafara mateka wake" kwa ajili ya "maslahi yake binafsi na ajenda za itikadi kali." 

Benjamin Netanyahu

Hamas imetoa wito kwa nchi za Kiarabu na Kiislamu na jamii ya kimataifa "kulaani na kupinga matamshi hatari ya Netanyahu na kuchukua hatua za haraka kukomesha uchokozi na kukomesha uvamizi huo."

Benjamin Netanyahu, ambaye anatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na anasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, alifichua katika mahojiano na Fox News kwamba ana nia ya kulikalia kwa mabavu eneo la Ukanda wa Gaza, na kulikabidhi kwa majeshi ya Kiarabu ambayo, kama alivyoeleza, si tishio kwa Israel.

Mapema leo Ijumaa pia Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, imetangaza kwamba baraza la mawaziri la usalama limeidhinisha pendekezo la kuudhibiti mji wa Gaza kama sehemu ya mpango mpana wa kukalia kwa mabavu Ukanda mzima.