Israel yasaini makubaliano ya kihistoria ya kuiuzia Misri gesi yenye thamani ya dola bilioni 35
Utawala wa kizayuni wa Israel umetangaza kusainiwa mkataba mkubwa utakaogharimu dola bilioni 35 wa kuiuzia Misri gesi asilia, unaotajwa kuwa ni "mkubwa zaidi katika historia ya Israel". Hayo yameelezwa na Eli Cohen, waziri wa nishati wa utawala huo ghasibu.
Kampuni ya NewMed Energy, ambayo ni m'bia katika eneo la gesi la Leviathan la Palestina inayokaliwa kwa mabavu, imesema mpango huo unajumuisha uuzaji wa takriban mita za ujazo bilioni 130 za gesi asilia kwa Misri utakaoendelea hadi mwaka 2040, au hadi pale kitakapokuwa kimekabidhiwa kiwango kamili kilichoafikiwa katika kandarasi.
Katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii siku ya Alkhamisi, Cohen alisema, kutia saini mkataba mkubwa zaidi wa gesi katika historia ni maendeleo muhimu katika masuala ya usalama, siasa na uchumi ya utawala wa kizayuni.
Aliongeza kuwa, hilo linaimarisha nafasi ya Israel kama nguvu inayoongoza ya nishati ya kikanda inayotegemewa na kuhitajiwa na nchi majirani. Na kwamba ni habari njema pia kwa uchumi, kwa sababu mabilioni ya dola yataingia kwenye hazina ya serikali, ajira mpya zitaandaliwa, na uchumi utapewa msukumo.
Mamlaka ya utangazaji ya umma ya utawala wa kizayuni imeripoti habari hiyo na kusema: "mkataba huu unakuja ukijumuishwa na makubaliano ya awali ya yaliyotiwa saini na Misri mwaka 2019, ambayo yalihusisha usafirishaji wa mita za ujazo bilioni 60, kumaanisha kwamba kiasi cha mauzo ya nje kuelekea Misri kitaongezeka mara tatu".../