Marekani yaiomba Russia isaidie kumaliza mzingiro Aleppo
-
Samantha Power
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ameiomba Russia itumie ushawishi wake ili kuvunja mzingiro katika mji wa Aleppo.
Katika hali ambayo Russia inaituhumu Washington kwa kulifanya la kisiasa suala la utoaji misaada ya kibinadamu kwa raia wa Syria, bi Samantha Power Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ameiomba Moscow kutumia ushawishi wake ili kuvunja mzingiro katika mji wa Aleppo huko Syria.
Samantha Power amesema kuwa Baraza la Usalama linapasa kuwaruhusu raia kupatiwa misaada ya kibinadamu katika pande mbili zote za mji wa Aleppo. Wakati huo huo bi Power ameashiria takwimu za UN zilizobainisha madai ya uwongo na kueleza kuwa serikali ya Syria ni masuuli katika kuzingirwa asilimia 80 ya maeneo nchini humo.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amedai pia kuwa kwa mara nyingine tena wanaitaka Russia itumie ushawishi wake kuishinikiza serikali ya Syria ihitimishe mzingiro katika maeneo yote ya nchi hiyo.
Wakati huo huo Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa amezituhumu Washington na waitifaki wake wa Magharibi kuwa wameligeuza kuwa la kisiasa suala la utoaji misaada ya kibinadamu kwa raia huko Syria na kuitaka Marekani na waitifaki wake kukiri kuwa, matatizo ya kibinadamu huko Syria hayana uhusiano wowote na harakati za kuendesha vita dhidi ya ugaidi za serikali halali ya Damascus.