UNRWA: Kuna kizazi kinaangamizwa Gaza
-
Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA)
Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa Ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza kuwa, watoto huko Gaza wanakufa kwa njaa, na kutochukua hatua na kunyamaza mbele ya jinai za utawala wa Israel ni sawa na kushiriki katika jinai hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Anadolu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Kazi kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limekosoa kimya na kutochukua hatua jamii ya kimataifa mbele ya jinai za utawala wa kizayuni wa Israel.
Shirika la UNRWA limeandika kwenye ukurasa wake rasmi kwenye mtandao wa kijamii wa "X" (zamani wa Twitter): "Kutochukua hatua na kunyamaza ni kuwa mshirika katika uhalifu. Ni wakati wa matamshi kutafsiriwa kwa vitendo na usitishaji mapigano mara moja uanzishwe."
Shirika hilo liliongeza: "Watoto huko Gaza wanakufa kwa njaa na mabomu. Familia nzima, vitongoji na kimsingi kuna kizazi kinachoangamiazwa huko Gaza."
Wakati huo huo, asasi mbalimbali zenye mfungamano na Umoja wa Mataifa na za ndani zimeendelea kutahadharisha kuwa, ipo hatari ya kushuhudiwa vifo vingi miongoni mwa watoto wa Ukanda wa Gaza iwapo mzingiro dhidi ya ukanda huo utaendelea na misaada ya kibinadamu itazuiwa kuingia katika eneo hilo.
Hali ya mambo kwa upande wa afya na maisha imezorota sana huku mfumo wa afya ukisambaratika kikamilifu huko Gaza.
Licha ya malori yaliyobeba misaada kurundikana katika lango la Ukanda wa Gaza, lakini utawala ghasibu wa Israel unaendelea kuzuia kuingia malori hayo huko Gaza nje ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.