Umoja wa Mataifa waonya juu ya kuibuka magonjwa ya kuambukiza Gaza
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, kushadidi wimbi la joto na kuendelea mashambulizi ya utawala ghasibu wa kizayuni kutapelekea kuenea magonjwa ya kuambukiza katika Ukanda wa Gaza.
Kituo cha Habari cha Palestina kimetangaza kuwa, huku wimbi la joto likizidi na utawala ghasibu wa Kizayuni ukiendelea na mashambulizi, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada yanatahadharisha kuhusu kuenea magonjwa ya kuambukiza katika Ukanda wa Gaza.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza kuwa, vituo vyake vya matibabu hupokea wastani wa wagonjwa 10,300 wanaougua magonjwa ya kuambukiza kila wiki, hasa kuhara kunakosababishwa na unywaji wa maji machafu.
Kulingana na mashirika ya misaada, kiwango cha maji cha kila siku kwa kila mtu huko Gaza ni chini ya lita tatu, kiwango ambacho ni cha chini sana ikilinganishwa na kiwango cha kimataifa ambacho ni lita 15, ambacho ni muhimu kwa ajili ya kunywa, kupikia na usafi. Vizuizi vya vya utawala wa kizayuni wa Israel kwa uagizaji wa mafuta na umeme vimesimamisha au kupunguza sana uwezo wa mitambo ya kusafisha maji huku uharibifu wa miundombinu na bomba kuu, ukipunguza ufikiaji wa watu kwa maji salama.
Munzer Shablaq, Mkuu wa Mamlaka ya Maji ya Manispaa ya Sahel huko Gaza, amesisitiza kwamba, uzalishaji wa maji ya kunywa umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na kabla ya vita, na kwamba kuweka kipaumbele kwa utoaji wa maji katika hospitali wakati mwingine kunakuja kwa gharama ya kusimamisha mifumo ya maji taka, suala ambalo linaongeza hatari ya uchafuzi wa mazingira na mrundikano wa taka katika vitongoji.