Ripoti: Watu wenye ulemavu wazidi kuongezeka Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129670-ripoti_watu_wenye_ulemavu_wazidi_kuongezeka_gaza
Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Mediterranean Human Rights Watch limeonya kuhusu ongezeko la watu wenye ulemavu katika vita vya Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-08-18T06:58:16+00:00 )
Aug 18, 2025 04:44 UTC
  • Kuna ongezeko la watu wenye ulemavu katika vita vya Ukanda wa Gaza vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel
    Kuna ongezeko la watu wenye ulemavu katika vita vya Ukanda wa Gaza vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel

Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Mediterranean Human Rights Watch limeonya kuhusu ongezeko la watu wenye ulemavu katika vita vya Ukanda wa Gaza.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Euro-Mediterania imeonya kuwa, vita vya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza vinasababisha ulemavu wa kudumu au wa muda kwa makumi ya Wapalestina kila siku.

Ripoti hiyo inabainisha kwamba, baada ya vita kumalizika, Ukanda wa Gaza utakabiliwa na kizazi cha walemavu ambao watahitaji msaada wa muda mrefu, huku miundombinu ya afya katika eneo hilo ikiharibiwa kabisa.

Sehemu nyingine ya taarifa ya shirika hilo la haki za binadamu inasema: Vita vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza vinawaacha Wapalestina 30 na ulemavu wa kudumu au wa muda kila siku.

Idadi ya walemavu katika Ukanda wa Gaza imeongezeka kwa takriban 35% wakati wa vita vya miezi 22 ikilinganishwa na kabla ya vita kuanza.

Kati ya takriban watu 165,000 waliojeruhiwa tangu kuanza kwa vita, kesi 21,000 za ulemavu wa kudumu na wa muda zimerekodiwa na Euro-Mediterranean Human Rights Watch.

Kadhalika makumi ya Wapalestina walemavu wametiwa mbaroni na jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel baada ya operesheni ya kijeshi ya jeshi la utawala huo ghasibu. Walemavu hao wanaishi katika mazingira yasiyofaa na wanakabiliwa na mateso, na hakuna habari kuhusu hatima yao.