WFP: Watu nusu milioni wako kwenye ukingo wa njaa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129676-wfp_watu_nusu_milioni_wako_kwenye_ukingo_wa_njaa_gaza
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, watu nusu milioni wako kwenye ukingo wa njaa katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.
(last modified 2025-08-18T07:07:16+00:00 )
Aug 18, 2025 07:07 UTC
  • WFP: Watu nusu milioni wako kwenye ukingo wa njaa Gaza

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, watu nusu milioni wako kwenye ukingo wa njaa katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.

Shirika hilo limesisitiza kuwa, usitishaji mapigano ndio njia pekee ya kupanua wigo wa upelekaji na usambazaji misaada katika eneo hili linalokabiliwa na mzingiro wa Israel.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani lilmeandika katika chapisho katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba kiasi cha misaada inayofika Gaza bado kiko chini sana ya kiwango cha mahitaji.

Msaada huo unaweza kuhudumia 47% pekee ya lengo la kila siku la mpango huo. Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imetabiri uwezekano wa kufikia vifo 500 kila siku kutokana na njaa.

Munir Al-Barsh, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, amsema kuwa watu 240 katika eneo hilo wameuawa shahidi kutokana na njaa na utapiamlo, 106 kati yao ni watoto, na kusema: "Ikiwa njaa itaendelea, tutakuwa kwenye hatua ambayo watu 500 watakufa kila siku."

Mashirika ya kimataifa ya misaada na haki za binadamu pia yameripoti juu ya kuendelea kuzuia utawala wa Kizayuni mchakato wa misaada ya kuingia Ukanda wa Gaza, mashambulizi ya makusudi ya utawala huo dhidi ya vikosi vinavyotoa usalama kwa misafara ya misaada, na kuuawa shahidi Wapalestina wasiopungua 1,769 kwa kupigwa risasi na jeshi la Kizayuni wa Israel walipokuwa wakisubiri kupokea misaada.