Marekani kuondoa wanajeshi wake Iraq kufikia mwisho wa Septemba
Wairaqi kutoka makundi na mirengo mbalimbali wamekuwa wakingoja kwa hamu kuondoka kikamilifu kwa majeshi ya Marekani nchini humo na sasa imebainika kuwa wataondoka mwisho wa Septemba.
Katika miaka iliyopita, kumekuwa na matamko kadhaa kuhusu uondoaji wa wanajeshi hao, lakini yote yamekuwa bure. Sasa, mshauri wa Waziri Mkuu wa Iraq ametoa taarifa akisema kwamba wanajeshi wa Marekani wataondoka katika ardhi ya Iraq kufikia mwishoni mwa Septemba. Hata hivyo, baadhi ya maafisa wanasema vikosi hivyo vitahamia kaskazini mwa Iraq badala ya kuondoka kikamilifu nchini humo.
Marekani kila mara imekuwa ikitoa matamko kuhusu kuondoka nchini Iraq, jambo ambalo limekuwa likizungumziwa tangu baada ya kutangazwa ushindi dhidi ya magaidi wa Daesh mnamo mwaka 2017.
Hata mwaka 2020 walizungumza kuhusu kubadili jukumu lao na kuingia katika awamu ya ushauri, wakiwa na idadi ndogo ya wanajeshi.
Mwaka uliopita, Waziri wa Ulinzi wa Iraq, Thabet Muhammad Saeed al-Abbas, alitangaza kuwa Wamarekani wangeondoka kwenye kambi zilizoko Baghdad na maeneo mengine, isipokuwa eneo la Kaskazini mwa Kurdistan, kufikia Septemba 2025.
Hata hivyo, haijawa wazi iwapo vikosi vya Marekani vitaondoka kabisa nchini humo kulingana na sheria iliyopitishwa na Bunge la Iraq.
Taarifa ya Ubalozi wa Marekani pia ilidai kuwa jukumu la muungano nchini Iraq litabadilishwa na kuwa ushirikiano wa kiusalama unaoongozwa na raia kati ya pande mbili, baada ya Bunge la Iraq kuitaka serikali kuondoa majeshi yote ya kigeni katika ardhi ya nchi hiyo kwa hoja kwamba yanahatarisha mamlaka ya Iraq.
Wairaqi wanataka nchi yao itegemee majeshi yake pekee katika kulinda mamlaka na umoja wa kitaifa.
Kumekuwa na mwito mkubwa wa wananchi, mara nyingi ukiwakilishwa kupitia maandamano na nyimbo za mitaani, wakitaka kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani ili Iraq ipate mamlaka kamili.
Kwa Wairaqi wengi, hili si suala la kisiasa pekee, bali pia ni jambo la heshima na utu, na kusitisha uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya nchi yao.