Mwanasoka mwingine wa Palestina auawa na Israel, FIFA yaendelea kuwa kimya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129906-mwanasoka_mwingine_wa_palestina_auawa_na_israel_fifa_yaendelea_kuwa_kimya
Mchezaji mwingine wa soka Palestina ameuawa shahidi na jeshi la utawala ghasibu wa Israel akiwa katika safu ya chakula cha msaada huku Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) likiendelea kukaa kimya.
(last modified 2025-08-23T23:26:34+00:00 )
Aug 23, 2025 23:26 UTC
  • Mwanasoka mwingine wa Palestina auawa na Israel, FIFA yaendelea kuwa kimya

Mchezaji mwingine wa soka Palestina ameuawa shahidi na jeshi la utawala ghasibu wa Israel akiwa katika safu ya chakula cha msaada huku Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) likiendelea kukaa kimya.

Vyanzo vya habari viliripoti kuuawa shahidi mmoja wa wachezaji wa timu ya soka ya Al-Jazeera wakati wa mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya foleni ya kusubiria chakula cha msaada kaskazini mwa Gaza.

Vyanzo vya habari vilitangaza kuwa Muhannad Jamal Alian, mchezaji wa timu ya soka ya Al-Jazeera, ameuawa shahidi kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Duru hizo pia zimetangaza kuwa, mwanasoka huyo kijana wa Kipalestina pamoja na raia wengine wa Palestina walikuwa wamesimama kwenye foleni wakisubiri kupokea misaada ya kibinadamu wakati alipolengwa na utawala wa Israel katika kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kuuawa shahidi.

Hivi karibuni nahodha na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Palestina Suleiman al-Obeid, anayejulikana kama Pele wa soka ya Palestina aliuawa shahidi katika shambulizi la kinyama la utawala wa kizayuni wa Israel alipokuwa akisubiri msaada wa chakula huko Gaza. Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufukuzwa timu za michezo za utawala wa Kizayuni katika mashindano ya kimataifa.

Katika miezi ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni kwa kutumia kisingizio cha "utaratibu wa kutoa misaada ya kibinadamu" uliobuniwa na Marekani kwa ushirikiano wa Tel Aviv, umewaelekeza Wapalestina masikini katika maeneo maalumu ya Ukanda wa Gaza na kisha kuwafyatulia risasi na kulipua mabomu kwa mpangilio.

Katika visa kadhaa, makumi ya Wapalestina wanaopanga foleni kwa ajili ya chakula na misaada ya matibabu wamekuwa wakilengwa moja kwa moja na wavamizi au mashambulizi ya ndege zisizo na rubani. Mashirika ya haki za binadamu yameelezea hatua hii ya ukatili kama "mtego wa kifo".