Askari wa Israel wamuua kamanda wao huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129918-askari_wa_israel_wamuua_kamanda_wao_huko_gaza
Mabomu yaliyotegwa na askari wa kikosi kimoja cha jeshi la Israel ili kuwaua Wapalestina yamemuangamiza kamanda wa kikosi hicho mwenyewe kusini mwa Gaza.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Aug 24, 2025 04:17 UTC
  • Askari wa Israel wamuua kamanda wao huko Gaza

Mabomu yaliyotegwa na askari wa kikosi kimoja cha jeshi la Israel ili kuwaua Wapalestina yamemuangamiza kamanda wa kikosi hicho mwenyewe kusini mwa Gaza.

Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kisa hicho Jumamosi, vikimtaja kamanda huyo kama Luteni Ori Gerlic aliyekuwa na umri wa miaka 20 kutoka Kikosi cha Shimshon cha Brigedi ya Kfir ya jeshi la Israel.
Kwa mujibu wa jeshi, Gerlic aliuawa katika jiji la Khan Younis, wakati bomu lilipolipuka katika eneo alilokuwa akifanya kazi wakati wa operesheni dhidi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas,  huko Gaza.
Kifo hicho kilitangazwa baada ya idhini kupatikana kutoka kwa Idara ya kubana habari za jeshi, ambayo huwa na jukumu la kuficha vifo vya askari wa Israel vitani.
Jeshi limeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo ambalo limeongeza idadi ya vifo vya wanajeshi kutokana na kile ambacho utawala unakiita, “ajali za kijeshi,” hadi kufikia 73.
Tukio hilo limechochea hasira kutoka kwa Wazayuni, ambao tayari wamepoteza mateka takriban 20 waliotekwa Gaza kutokana na mashambulio ya jeshi la Israel ambayo hayakuwa na mpangilio.

Jeshi limesema kuwa wanajeshi wake wapatao 899 wameuawa tangu Oktoba 2023, wakati utawala huo ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.
Hata hivyo, makadirio mengi yanaelezea idadi hii kuwa kubwa zaidi ya iliyotangazwa rasmi kwani kumekuwa na juhudi kubwa za kubana taarifa za askari Waisraeli waliouawa vitani kwa hofu ya kushusha wasiwasi jeshini.

Jeshi la Israel hutekeleza sera  inayojulikana kama “Itifaki ya Hannibal” inayohimiza majeshi ya Israel kuwapiga risasi na kuwaua wenzao ikiwa watatekwa, kwa madai kuwa askari aliyekufa ni bora kuliko yule aliye hai lakini ametekwa.