Tangu Agosti 6, jeshi la Israel limebomoa kikamilifu majengo zaidi ya 1,000 ya Mji wa Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129972-tangu_agosti_6_jeshi_la_israel_limebomoa_kikamilifu_majengo_zaidi_ya_1_000_ya_mji_wa_ghaza
Shirika la Ulinzi wa Raia la Palestina limetangaza kuwa jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel limebomoa kikamilifu majengo zaidi ya 1,000 katika vitongoji vya Zeitoun na Sabra katika Mji wa Ghaza tangu lilipoanza kuuvamia mji huo mnamo Agosti 6, na hivyo kupelekea mamia ya Wapalestina kunasa chini ya vifusi vya majengo hayo.
(last modified 2025-10-15T09:12:33+00:00 )
Aug 25, 2025 06:59 UTC
  • Tangu Agosti 6, jeshi la Israel limebomoa kikamilifu majengo zaidi ya 1,000 ya Mji wa Ghaza

Shirika la Ulinzi wa Raia la Palestina limetangaza kuwa jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel limebomoa kikamilifu majengo zaidi ya 1,000 katika vitongoji vya Zeitoun na Sabra katika Mji wa Ghaza tangu lilipoanza kuuvamia mji huo mnamo Agosti 6, na hivyo kupelekea mamia ya Wapalestina kunasa chini ya vifusi vya majengo hayo.

Shirika hilo limeeleza katika taarifa kwamba mashambulio yanayoendelea kufanywa na jeshi la kizayuni na uzibaji njia linaofanya vinakwamisha shughuli nyingi za uokoaji na utoaji msaada katika eneo hilo.

Taarifa ya shirika la ulinzi wa raia la Palestina imeendelea kueleza kwamba, wafanyakazi wa huduma za dharura wanaendelea kupokea ripoti nyingi za watu waliopotea lakini wanashindwa kuchukua hatua yoyote, huku hospitali zikielemewa na idadi ya majeruhi wa mashambulizi hayo.

"Kuna wasiwasi mkubwa kutokana na kuendelea uvamizi wa vikosi vya Israel katika Mji wa Ghaza, huku wafanyakazi wa ugani wakiwa wanakosa uwezo wa kukabiliana na ukubwa wa mashambulizi yanayoendelea ya Israel," imebainisha taarifa ya shirika hilo.

Taarifa hiyo imetoa indhari kwa kusema: "hakuna eneo salama katika Ukanda wa Ghaza, iwe ni kaskazini au kusini, ambapo mashambulizi ya makombora yanaendelea kuwalenga raia majumbani mwao, kwenye hifadhi na hata katika kambi zao".

Vifaru vya jeshi la utawala wa kizayuni vimekuwa vikiingia ndani ya kitongoji cha Sabra kwa azma ya kuukalia kikamilifu Mji wa Ghaza, na kuwalazimisha karibu Wapalestina milioni moja wahame kuelekea kusini.

Taarifa ya shirika la Ulinzi wa Raia inathibitisha hofu ya kwamba utawala ghasibu wa Israel unapanga kuubomoa kikamilifu Mji wa Ghaza, kama ulivyofanya huko Rafah, kampeni ambayo watetezi wa haki wanasema inaweza kuwa na lengo la kuwaondoa Wapalestina wote katika Ukanda wa Ghaza.

Wakati huohuo, janga la njaa ya kutengenezwa na Israel limekatisha maisha ya Wapalestina wengine wanane, akiwemo mtoto mdogo.

Munir al-Bursh, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Ghaza amesema vifo hivyo vimeifanya idadi ya waliofariki kutokana na lisheduni tangu Oktoba 2023 hadi sasa kufikia 289, wakiwemo watoto 115.

Tangu wakati huo hadi sasa Jeshi la utawala wa kizayuni limeshawaua shahidi Wapalestina zaidi ya 62,600 huko Ghaza.../