Je, inatosha kwa nchi za Magharibi kulaani kwa maneno matupu jinai za utawala wa Israel?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i129990-je_inatosha_kwa_nchi_za_magharibi_kulaani_kwa_maneno_matupu_jinai_za_utawala_wa_israel
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 21 za Magharibi kwa pamoja wamelaani uamuzi wa Israel wa kujenga makaazi mapya ya walowezi wa Kizayuni huko Quds Mashariki.
(last modified 2025-08-26T02:42:48+00:00 )
Aug 26, 2025 02:42 UTC
  • Je, inatosha kwa nchi za Magharibi kulaani kwa maneno matupu jinai za utawala wa Israel?

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 21 za Magharibi kwa pamoja wamelaani uamuzi wa Israel wa kujenga makaazi mapya ya walowezi wa Kizayuni huko Quds Mashariki.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na Uingereza, Australia na Japan katika taarifa yao siku ya Ijumaa, huku wakilaani mpango wa Wazayuni wa kuendeleza vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Quds Mashariki, wameutangaza uamuzi huo kuwa "usiokubalika," ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kutaka ufutiliwe mbali mara moja. Mawaziri hao wameonya katika taarifa yao kwamba mpango huo "utafanya suluhisho la serikali mbili lisiwezekane" na kubana ufikiaji wa Wapalestina huko Beitul Muqaddas.

Nchi zilizochangia taarifa hii ni pamoja na Australia, Ubelgiji, Uingereza, Canada, Cyprus, Denmark, Estonia, Finland, Ufaransa, Ugiriki, Iceland, Ireland, Italia, Japan, Latvia, Lithuania, Luxembourg, Malta, Uholanzi, Norway, Poland, Ureno, Slovenia, Hispania na Uswidi. Kaya Callas, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya, pia alijiunga na taarifa hii.

Siku ya Jumatano, utawala wa Kizayuni uliidhinisha mpango wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika eneo la (E1) mashariki mwa Beitul Muqaddas kwa lengo la "kuvuruga umoja wa ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan" na "kubuniwa nchi ya Palestina". Mpango huu uliidhinishwa na kamati ya makazi ya Wazayuni inayoongozwa na Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha wa utawala huo. Kwa kutekelezwa mradi huu, ambao unatenganisha kabisa kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na eneo la Kusini, nyumba mpya 3,400 zitajengwa kwa ajili ya Wazayuni. Katika kikao hicho, Smotrich aliuita mpango wa kuunganisha mji wa "Ma'ale Adomim" na Beitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu na hivyo kukata umoja wa ardhi ya Ukingo wa Magharibi kati ya "Ramallah" na "Beitul Muqaddas" kama "msumari wa mwisho kwenye jeneza" la wazo la kuunda taifa la Palestina na kusema: "Nchi ya Palestina inatoweka; si kwa maneno tu bali kwa vitendo." Kuhusiana na mpango huu, Wazayuni wanadai kwamba "haki ya kihistoria ya Wayahudi kuishi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ni jambo lisilopingika" na kwamba vitendo vyao vinaendana na sheria za kimataifa.

Tangu mwaka 1967, Israel imekalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi, Beitul Muqaddas Mashariki na Gaza, na sambamba na kuendesha vita na Hamas katika Ukanda wa Gaza, imepanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Hivi sasa, walowezi wapatao 700,000 wa Israel wanaishi kati ya Wapalestina milioni 2.7 katika Ukingo wa Magharibi na Beitul Muqaddas Mashariki.

Maandamano ya kuunga mkono Palestina kimataifa

Hii ni katika hali ambayo, hatua ya nchi za Magharibi ya kulaani kwa maneno tu hatua za utawala wa Kizayuni katika kuendeleza vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizotekwa mwaka 1967, si tu hakuzuii hujuma za wazi za Israel dhidi ya nyumba, mashamba na suhula za Wapalestina, bali kimsingi hakutoi kipingamizi chochote dhidi ya utawala wa Kizayuni cha kuuzuia kuendeleza harakati zake za kujitanua katika ardhi za Wapalestina.

Misimamo mipya ya nchi za Magharibi dhidi ya Israel, kwa kutilia maanani kuendelea na kupanuka hatua za chuki na ulowezi wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, hususan uendelezaji wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na wakati huo huo  kuendesha mauaji ya kimbari na kutumia njaa kama silaha pamoja na kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia katika Gaza kwa lengo la kuangamiza na kuwalazimisha wakazi wahame na kuacha nyumba zao, inathibitisha wazi kumalizika na kudhoofika nguvu laini ya ushawishi wa utawala haramu wa Israel katika nchi za Magharibi, katika kuhalalisha vitendo vyake vya jinai dhidi ya watu wanaodhulumiwa huko Gaza.

Kwa hakika jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza na hatua zake haramu dhidi ya Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ziko wazi kabisa na wala hazifichiki kiasi kwamba nchi za Magharibi hazina budi ila kulaani angaa kidhahiri tu hatua za Israel kutokana na uungaji mkono mkubwa wa kimataifa kwa wananchi kwa Wapalestina. Pamoja na hayo nchi hizi, hasa za Ulaya, hazichukui hatua yoyote ya maana na ya kivitendo kwa ajili ya kuzuia vitendo vya uchokozi na jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Nukta muhimu ni kwamba, Wamagharibi kimsingi ni waungaji mkono na watetezi wakubwa wa Israel, na hata mwanzoni mwa vita vya Gaza, baadhi ya viongozi wa Ulaya walisafiri hadi Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa ajili ya kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza. Hata hivi sasa, hatua hii ya nchi za Magharibi, kwa kuzingatia uhusiano mkubwa uliopo kati ya baadhi ya nchi za Ulaya ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya na utawala huo, kama vile Ujerumani, Hungary na Jamhuri ya Czech, kwa kiasi kikubwa ni vitendo vya kimaonyesho tu, propaganda na unafiki wa wazi. Kama ambavyo katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya, kati ya nchi 27 wanachama wa umoja huo, wanachama 10 wa umoja huo walipinga kutazamwa upya mapatano ya ushirikiano wa kibiashara na Israel na hivyo kuonyesha wazi mshikamano wao wa kivitendo na utawala huo wa Kizayuni.