Wanajeshi wengine sita wa Israel waangamizwa na kujeruhiwa huko Ghaza
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kutokea tukio zito la kiusalama kwa wanajeshi wa utawala huo dhalimu huko kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, kwa mujibu wa tovuti ya lugha ya Kiebrania ya Hadashot Bazman, vikosi vya Hamas vilishambulia kambi ya kijeshi ya Israel huko kusini mwa Ukanda wa Ghaza kwa roketi za RPG na bunduki asubuhi ya leo, Jumanne.
Hadashot Bazman ameongeza kuwa, katika operesheni hiyo, mwanajeshi mmoja wa Israel ameangamizwa na wengine watano kujeruhiwa, baadhi yao wakiripotiwa kuwa katika hali mahututi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kizayuni, wanajeshi wa Israel waliojeruhiwa walihamishwa kwa helikopta hadi hospitali za Soroka na Sheba.
Mwezi uliopita wa Septemba, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS iliuonya utawala wa kizayuni wa Israel kwamba hatua yake ya kuzidi kujiingiza ndani ya Mji wa Ghaza itaugeuza mji huo kuwa "kaburi," la wanajeshi wa kizayuni baada ya sita miongoni mwao kuangamizwa na wanamuqawama wa Palestina katika matukio tofauti wakati wa jeshi la Israel likiwa linaendeleza mashambulizi ya kinyama yanayolenga kulikalia kwa mabavu eneo lote la Ghaza.
Tawi la kijeshi la Hamas la Izzuddinul-Qassam, limeeleza katika taarifa yake kwamba Ghaza ni "vita vya msuguano vyenye gharama kubwa" na kuonya kwamba hatima ya mateka wa Israel inategemea harakati za kijeshi za utawala huo wa kizayuni.
Taarifa hiyo ya Al-Qassam iliyotolewa kwa Kiebrania imesisitiza kuwa wapiganaji wa Hamas wamesambazwa katika vitongoji vyote vya Ghaza, wakiwa tayari kukabiliana na jeshi la utawala ghasibu wa Israel.