Ulaya haina haki ya kutoa maoni kuhusu uwezo wa kiulinzi wa Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepinga vikali madai ya uingiliaji kati na yasiyo na msingi ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Umoja wa Ulaya, alkiwaonya viongozi wa nchi za Ulaya na Magharibi kwamba hawana haki ya kusema chochote kuhusu uwezo wa kiulinzi wa Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, taarifa ya pamoja ya kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Umoja wa Ulaya na ndani yake kutolewa madai yasiyo na msingi, yakiwemo kuhusu visiwa vitatu vya Iran na mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, imepata majibu makali kutoka kwa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei.
Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi linaloundwa na nchi Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Kuwait, Oman na Qatar na Umoja wa Ulaya zilitoa taarifa jana, Jumatatu (Oktoba 6), katika mkutano wao wa 29 wa pamoja. Taarifa hiyo ilisisitiza kusitishwa mpango wa makombora wa Iran na kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Leo Jumanne Oktoba 7, Esmael Baghaei amepinga vikali madai hayo ya kuingilia kati na yasiyo na msingi yaliyotolewa katika taarifa ya pamoja ya kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na kurudiwa madai ya Muungano wa Falme za Kiarabu kuhusu visiwa vya Iran vya Tomb Kubwa, Tomb Ndogo, na Buu Musa na kusisitiza kuwa nchi zozote zile hasa za Magharibi hazipaswi kujipa mamlaka ya kuzungumzia nguvu za kiulinzi za Iran.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje, amesisitiza tena kwamba visiwa hivyo vitatu ni sehemu ya ardhi ya Iran isiyoweza kutenganishwa na maeneo mengine ya Jamhuri ya Kiislamu.